IQNA

WFP: Ugavi wa chakula Gaza haujafikia wanaohitaji zaidi

17:00 - October 22, 2025
Habari ID: 3481401
IQNA – Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) limesema kuwa kiwango cha chakula kinachoingia Gaza bado kiko chini sana ya lengo la tani 2,000 kwa siku, likitoa wito kwa utawala wa Kizayuni kufungua vituo zaidi vya mipakani.

WFP imesema kuwa ugavi wa chakula umeongezeka baada ya kusitishwa kwa mapigano, lakini bado haujafikia kiwango kinachohitajika kwa sababu ni vituo viwili tu vya kuingia katika eneo la Palestina vinavyofanya kazi.

Kwa mujibu wa WFP, takriban tani 750 za chakula zinaingia Ukanda wa Gaza kila siku, lakini kiwango hicho bado ni kidogo sana ikilinganishwa na mahitaji makubwa baada ya vita vya miaka miwili vilivyoharibu sehemu kubwa ya Gaza.

“Ili kufanikisha ongezeko hili, tunapaswa kutumia kila kituo cha mipaka kilichopo kwa sasa,” alisema msemaji wa WFP, Abeer Etefa, katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Geneva siku ya Jumanne.

Alisema ni vituo viwili tu vinavyodhibitiwa na utawala wa Kizayuni vinavyofanya kazi , Karem Abu Salem kusini na al-Karara katikati ya Gaza.

Etefa alisisitiza kuwa kudumisha usitishaji wa mapigano ni “muhimu sana; kwa kweli, ni njia pekee ya kuokoa maisha na kupunguza njaa kali kaskazini mwa Gaza.”

Msemaji huyo alisema kuwa shirika hilo la UN sasa lina vituo 26 vya usambazaji wa chakula vilivyofunguliwa Gaza , kutoka vituo 5 tu siku ya Ijumaa , lakini bado ni chini sana ya vituo 145 vinavyolengwa kuanzishwa katika eneo lote. Vingi vipo kusini na katikati ya Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, alisema Jumamosi kuwa mpaka wa Rafah kati ya Gaza na Misri utaendelea kufungwa hadi taarifa nyingine, na kufunguliwa kwake kutategemea Harakati ya Hamas kukabidhi miili ya mateka waliokufa.

Hamas ilisema Jumanne kuwa itakabidhi miili ya mateka wawili wa Kizayuni. Katika taarifa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za Ezzedin al-Qassam,  limesema : “Tutakabidhi miili ya wafungwa wawili wa Kizayuni waliopatikana leo katika Ukanda wa Gaza saa 3 usiku kwa saa ya Gaza (18:00 GMT).”

Kundi hilo tayari limekabidhi miili 13 kati ya 28 waliokuwa wameahidi kuirejesha chini ya makubaliano ya awali.

Etefa alisema baadhi ya vifaa vya lishe kwa watoto na wanawake wajawazito vimefika kaskazini mwa Gaza kupitia kusini, lakini bado ni chini sana ya kiwango kinachohitajika.

“Hatujafanikiwa kupeleka misafara mikubwa ya misaada katika Jiji la Gaza au kaskazini mwa Gaza,” alisema, akiongeza kuwa WFP haijapewa ruhusa ya kutumia barabara kuu ya Salah al-Din inayounganisha kaskazini na kusini.

Chakula kilichopelekwa hadi sasa kinatosha kuwalisha takriban watu nusu milioni kwa muda wa wiki mbili, alisema. Wapalestina wengi wanahifadhi chakula wanachopokea kwa hofu kuwa ugavi unaweza kukatika tena.

“Wanatumia sehemu ya chakula hicho, na wanakigawa kwa tahadhari na kuhifadhi kwa dharura, kwa sababu hawana uhakika ni kwa muda gani usitishaji vita utadumu na nini kitatokea baadaye,” alisema.

3495103

 

captcha