IQNA

Sheikh Saleh Al-Fawzan Ateuliwa Mufti Mkuu Mpya wa Saudi Arabia

16:55 - October 23, 2025
Habari ID: 3481406
IQNA – Mwanazuoni mwenye msimamo wa kihafidhina na aliye katika miaka ya tisini ameteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa kidini au Mufti Mkuu nchini Saudi Arabia, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

Sheikh Saleh bin Fawzan bin Abdullah Al-Fawzan ametangazwa rasmi kuwa Mufti Mkuu wa Saudi Arabia kupitia amri ya kifalme, shirika rasmi la habari la SPA liliripoti Jumatano usiku.

Sheikh Al-Fawzan anachukua nafasi ya Sheikh Abdulaziz al-Asheikh, aliyekuwa Mufti Mkuu kwa zaidi ya miaka ishirini hadi alipofariki mwezi Septemba mwaka huu. Uteuzi wake umetokana na mapendekezo ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mohammed bin Salman, ambaye ndiye mtawala wa kiutendaji wa Saudi Arabia.

Uteuzi wa Sheikh Al-Fawzan haukushangaza, kwa mujibu wa Dkt. Umar Karim, mtaalamu wa sera za Saudi Arabia kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza. Akizungumza na shirika la habari la AFP, Dkt. Karim alisema: “Uteuzi huu unafuata sera ya kidini ya Saudi Arabia ya kumchagua mwanazuoni mwenye heshima kubwa na uzoefu wa muda mrefu ndani ya baraza la wanazuoni.”

Aliongeza kuwa ingawa mazingira ya kijamii yamebadilika na yanaendelea kubadilika, mifumo ya uendeshaji wa masuala ya kidini na namna yake ya kazi bado haijabadilika.

Sheikh Saleh Al-Fawzan, anayeheshimika sana katika muktadha wa elimu ya Sharia na fatwa, sasa anashika nafasi ya juu kabisa ya Kiislamu katika ufalme huo unaosimamia miji mitakatifu ya Makkah na Madinah, hadhi ambayo inaangaziwa kwa makini na ulimwengu wa Kiislamu.

3495122

Kishikizo: saudi arabia mufti
captcha