
Katika mahojiano na Al Jazeera Net, Dkt. Noura Bouhannache, profesa wa falsafa ya maadili katika Chuo Kikuu cha Constantine, alionya kuwa kasi ya “ukisasa (modernization) wa kulazimishwa” imebadilisha sura ya familia ya Kiislamu na kudhoofisha kiini chake cha kiroho.
Bouhannache alieleza kuwa jamii nyingi za Kiislamu sasa zinaiga mfano wa familia ya Kimagharibi “kwa sura ya kidini” lakini bila kiini chake cha kimaadili na kiroho.
“Tunashuhudia toleo la familia ya Kimagharibi lililovikwa vazi la kidini, lakini limepoteza maana yake ya ndani,” alisema.
Akizungumzia mijadala ya sasa kuhusu wanawake, Bouhannache aliweka hoja hiyo ndani ya historia pana ya fikra. Alifafanua kuwa fikra za kifeministi ziliibuka kama majibu kwa tafsiri za Kikristo na Aristotelian zilizowachora wanawake kama duni.
Alinukuu kauli ya Simone de Beauvoir: “Mwanamke huzaliwa si mwanamke, bali hujengeka kuwa mwanamke.” Akasema dhana hii iliwahimiza wanawake wa Magharibi kukataa majukumu ya jadi kama uzazi na ndoa, na kuingia katika maisha ya umma “kwa mapambano ya upande mmoja dhidi ya wanaume.”
Bouhannache aliongeza kuwa mitazamo ya kifeministi ya kisasa imeenda mbali zaidi kwa kudai tofauti za kijinsia ni za kijamii na si za kiasili, wazo linaloongeza mgongano badala ya kuleta maelewano.
Wanazuoni kama Abdelwahab El-Messiri, alibainisha, wanaona kuwa uanaharakati wa kifeministi unaakisi mwelekeo wa Magharibi wa kuachana na misingi ya kimaadili na kidini, na kupelekea “jumla ya kimaada iliyofichika.”
Bouhannache alisisitiza kuwa maadili ni ya asili, huku dini ikiyaimarisha na kuyapandisha daraja. Imani, alisema, hutoa msingi wa kimetafizikia unaopeleka matendo ya kimaadili kupata maana na mwongozo wa vitendo kupitia Qur’ani na Sunnah.
Alionya kuwa kuvunjika kwa maadili katika jamii nyingi za kisasa kunatokana na kupoteza vyote viwili.
Aidha, alieleza kuwa Waislamu wengi wanaishi katika “usekula uliopotoshwa,” wakitenganisha ibada za kidini na mwenendo wa kimaadili, na kutumia dini kwa manufaa ya kidunia. Hali hii, alisema, huzalisha “udini wa bandia” na kuchochea misimamo mikali kwa kukata uhusiano kati ya imani na tabia njema.
Kuhusu wanawake, Bouhannache alisema wanateseka kutokana na ukandamizaji wa kiume, lakini mara nyingi hutafuta ukombozi katika fikra za kifeministi za Magharibi, jambo linalochochea kuibuka kwa “ufeministi wa Kiislamu.” Hata hivyo, alibainisha kuwa juhudi za kuunganisha misingi ya kifeministi ya Magharibi na maandiko ya Kiislamu huleta migongano na kudhoofisha familia.
“Mgogoro wetu halisi ni mgogoro wa kumjenga binadamu,” alisisitiza.
Bila maadili thabiti, alisema, teknolojia, hasa akili bandia, inaweza kuongeza upweke ndani ya familia.
Suluhisho, alisisitiza, ni kujenga upya binadamu kupitia mfumo imara wa maadili utakaosaidia jamii kutumia teknolojia kwa hekima badala ya kumezwa nayo.
3495436