IQNA

Warsha Yemen kuhusu uhifadhi wa nyaraka za kale za Qur'ani Tukufu

16:08 - November 19, 2025
Habari ID: 3481538
IQNA – Warsha ya mafunzo kuhusu mbinu na njia za kuhifadhi na kukarabati nyaraka za kale za Qur'ani Tukufu za mwanzo imefanyika nchini Yemen.

Jengo la Nyaraka (Manuscripts House) lililoko Sana’a, mji mkuu, lilikamilisha warsha hiyo Jumatatu. Mpango huu uliandaliwa na Sekta ya Nyaraka na Maktaba chini ya Wizara ya Utamaduni na Utalii, kwa msaada wa Taasisi ya Kiutamaduni ya Imam Zaid bin Ali.

Warsha ya siku kumi ililenga kuwapa washiriki 30, wanaume na wanawake, ujuzi wa kuhifadhi, kukarabati, kufunga, kufunika na kushona nyaraka za kihistoria na parchments za Qur'ani Tukufu, pamoja na mbinu za kuzilinda dhidi ya kuharibika.

Katika hafla ya kufunga, Naibu Waziri wa Utamaduni na Utalii Abdullah Al-Washali alisisitiza umuhimu wa kuwapa washiriki utaalamu wa kukarabati na kuhifadhi nyaraka za kihistoria na za Kiislamu, ili kuhakikisha zinabaki salama, akizitaja kuwa sehemu muhimu ya urithi wa kihistoria na kiutamaduni wa Yemen.

Al-Washali alionyesha kuwa ni lazima kuhifadhi nyaraka zote, za kidini, kihistoria au kiakiolojia, kwani ndizo zinazoakisi historia na ustaarabu wa Yemen. Alithibitisha kuwa maendeleo ya taifa yanahusiana moja kwa moja na urithi wake wa kihistoria.

Aidha, alisisitiza dhamira ya Wizara ya Utamaduni kulinda nyaraka za kihistoria na za kidini dhidi ya kutelekezwa na kuharibika, akielekeza Jengo la Nyaraka kuzipa kipaumbele katika uhifadhi, ukarabati na matengenezo. Pia alieleza utayari wa Wizara kutoa msaada na rasilimali ili kulinda na kukarabati nyaraka kwa njia zinazoongeza utambulisho wa kiimani wa Yemen. Mwisho wa warsha, vyeti vya shukrani viligawiwa kwa washiriki.

3495433

Kishikizo: nyaraka qurani tukufu
captcha