
Mkutano huo ulizinduliwa katika ukumbi wa mikutano uliopo karibu na haram tukufu ya Ahmad ibn Musa (AS), anayejulikana kama Shah Cheragh, kwa ushiriki wa wanazuoni na watafiti wa ndani na wa kimataifa.
Mkutano huu umejikita katika matumizi ya akili mnemba (artificial intelligence) katika tiba na masomo yanayohusiana na afya ya kiroho pamoja na maadili ya kitabibu.
Akihutubia katika hafla ya ufunguzi, Hujjatul-Islam Ebrahim Kalantari, msimamizi wa haram ya Shah Cheragh (AS), alirejea umuhimu wa akili mnemba katika nyanja mbalimbali za sayansi zikiwemo tiba, na kuutaja kama hatua ya mabadiliko makubwa katika maendeleo ya kisayansi.
Alisisitiza kuwa siku zijazo, mashine zitaweza kuchambua na kutoa hitimisho, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto mpya kwa mwanadamu.
Alisema kuwa akili mnemba na teknolojia zote ni zao la mwanadamu, na mwanadamu mwenyewe ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu. “Hivyo, ni lazima tukumbuke daima kwamba kila kitu kilichopo duniani kinahesabika kwa namna moja au nyingine kuwa ni katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu.”
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mkutano huo, Mohammad Hadi Imanieh, katika hotuba yake alikumbusha historia ya kufanyika kwa mkutano huu kila baada ya miaka miwili tangu mwaka 2013.
Alisema maendeleo ya kisayansi katika utafiti wa mwili wa mwanadamu yanaongezeka kila siku, na leo hii, taaluma ya jeni (genetics) na mchango wake katika afya ya binadamu imepata umuhimu wa pekee, hali ambayo imepelekea maadili na masuala ya kiroho kupatiwa nafasi ndogo katika jamii.
Alieleza kuwa mkutano huu unalenga kukuza afya ya kiroho na maadili mema sambamba na kuendeleza sayansi.
Imanieh pia alisema kuwa kupitia akili mnemba, hifadhidata kubwa zinazohusiana na Qur’an Tukufu na Ahlul-Bayt (AS) zinaweza kuchambuliwa na kutumika katika nyanja ya afya ya akili na kiroho.
Hujjatul-Islam Abdolreza Mahmoudi, mkurugenzi wa mkutano huo, naye aliwahutubia washiriki akisema kuwa moja ya malengo makuu ya mkutano ni kuendeleza mafanikio ya kisayansi yanayochochewa na Sira ya Mtume (SAW).
“Tuna matumaini kuwa mkutano huu utaweza kufafanua dhana ya tiba ya kiroho na mafunzo ya kimaadili ndani ya jamii ya kitabibu nchini,” alisema.
Kwa mujibu wa katibu wa kisayansi wa mkutano huo, Mahmoud Nejabet, kati ya jumla ya makala 150 zilizowasilishwa, makala 119 zimekubaliwa kuwasilishwa kwa njia ya mabango (poster), na makala tano bora zaidi zitawasilishwa kwa njia ya mihadhara.
Aliongeza kuwa programu za mkutano huu zinajumuisha vipindi maalumu nane katika nyanja za historia ya tiba, tiba ya Kiislamu, maadili ya kitabibu, sayansi ya tabia na masomo ya kidini, pamoja na warsha tatu za taaluma mseto kwa lengo la kuimarisha ujuzi wa utafiti.
Nejabet pia alitaja ushiriki wa watafiti wa kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Duke nchini Marekani pamoja na nchi za Ugiriki na Lebanon, akieleza kuwa mchango wao unaonesha uwezo mpana wa mada ya Sira ya Mtume (SAW) kupanuka katika maeneo mapya ya afya na maadili ya kitabibu katika ngazi ya kimataifa.
4317926