IQNA

Mhubiri wa Al-Aqsa Sheikh Sabri asema kesi yalenga kuwanyamazisha watetezi wa Msikiti

17:49 - November 18, 2025
Habari ID: 3481536
IQNA – Sheikh Ekrima Sabri amesema mamlaka za Kizayuni zinapotosha dhana za Kiislamu kwa malengo ya kisiasa, wakati akikabiliwa na kesi mjini al-Quds kwa tuhuma za uchochezi.

Sheikh Sabri, mhubiri wa Msikiti wa Al-Aqsa, alizungumza na waandishi wa habari kabla ya kufikishwa mahakamani, akionya kuwa maafisa wa Israel “wanabadilisha fikra za Kiislamu zinazokubalika kwa Wapalestina na tafsiri za kisiasa zinazotumiwa na Israel.”

Alisema kauli za kidini anazotumia katika hotuba zake “zipo kama ilivyo katika Qur’ani na Sunnah,” na ni sehemu ya imani na jukumu lake la kidini. Aliongeza kuwa kauli hizi ni sehemu ya urithi wa muda mrefu na ana “haki ya kuitumia kwa uhuru.” Alisisitiza kuwa mahakama ya Israel “haina haki ya kutafsiri dhana hizi za Kiislamu kuwa eti ni za kisiasa au za uchochezi.”

Kesi Dhidi ya Sheikh Sabri

Mamlaka za Israel zimeandaa kumfikisha mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 86 mahakamani, ambapo mashtaka ya uchochezi yaliyowasilishwa na waendesha mashtaka wa umma yatapitiwa. Timu yake ya utetezi imesema tuhuma hizo zinahusiana na salamu za rambirambi alizotoa baada ya kuuawa kwa Ismail Haniyeh, aliyekuwa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, katika shambulio la kigaidi la Israel nchini Iran mwaka 2024, na pia kwa Wapalestina waliouawa na risasi za Israel katika Ukingo wa Magharibi mwaka 2022.

Sheikh Sabri alisema tayari amewahi kuhojiwa mara kadhaa kwa tuhuma za “uchochezi na kuunga mkono ugaidi,” ambazo hazikuthibitishwa. Aliongeza kuwa vyombo vya habari vya Israel na makundi yenye misimamo mikali vinaendelea kushinikiza mashtaka, hata kufikia kutoa “vitisho vya kifo sawa na vilivyotolewa dhidi ya Sheikh Ahmed Yassin.”

Lengo la Kuzuia Upinzani

Alisema vizuizi vinavyowekwa dhidi yake vinakusudia kunyamazisha wanamuqawama au wapigania ukombozi na kuwatisha Wapalestina katika jiji la al-Quds.

“Madhumuni yake ni kunyamazisha sauti za upinzani na kueneza hofu katika jamii ya al-Quds na Wapalestina kwa ujumla, ili kuzuia utetezi wa Msikiti wa Al-Aqsa na kupinga makundi yenye misimamo mikali yanayoharibu viwanja vyake,” alisema.

Sheikh Sabri aliongeza kuwa baadhi ya makundi ya Kiyahudi hufanya ibada za Kiyahudi na kucheza katika viwanja vya Msikiti wa Al-Aqsa bila kuwajibishwa, “kinyume na sheria kuhusu ugaidi na usalama.”

Hatua za Kuzuia na Ukandamizaji

Mamlaka za Israel tayari zilimzuia Sheikh Sabri kuingia Al-Aqsa kwa muda wa miezi sita. Timu yake ya utetezi imeeleza kesi hii kama sehemu ya “msururu wa hatua za kiholela na mateso ya kisiasa, kidini na kiitikadi,” ikiwemo marufuku ya kusafiri na amri ya kubomoa nyumba yake.

Wamesema mashtaka haya ni matokeo ya “kampeni kubwa ya uchochezi” inayosukumwa na maafisa wa mrengo wa kulia wa Israel.

Potovu Dhidi ya Viongozi wa Kidini

Tume ya Kiislamu-Kikristo ya Kuunga Mkono al-Quds imelaani kesi hii, ikieleza kuwa ni “shambulio la moja kwa moja dhidi ya wanazuoni na viongozi wa kidini” katika mji wa al  Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel. Katika taarifa yake, tume hiyo ilisema kesi hii ni sehemu ya sera ya kimfumo inayolenga “kunyamazisha na kuwazuia viongozi wa kidini,” na ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa ibada na maelezo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa lengo ni “kudhoofisha nafasi ya Kiislamu na Kiarabu na usimamizi wa ukoo wa Kihashimiyah juu ya Msikiti wa Al-Aqsa, na kufungua njia ya utawala wa walowezi.”

Tume hiyo ilisifu “msimamo wa kitaifa wenye ujasiri wa Sheikh Sabri” na kuzihimiza taasisi za Kiarabu na Kiislamu kuchukua hatua haraka “kukomesha kesi hii isiyo ya haki na kufichua ukiukaji wa uhuru wa kidini kama uhalifu wa kivita unaohitaji uwajibikaji wa kimataifa.”

3495442

Habari zinazohusiana
Kishikizo: sheikh sabri al aqsa
captcha