IQNA

Umuhimu wa Ayat al‑Kursi katika Qur’ani kwa mujibu wa mwanazuoni wa Misri

14:41 - May 05, 2026
Habari ID: 3482203
IQNA – Sheikh Khaled Al‑Jandi, mjumbe wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu nchini Misri, amesema kuwa, kwa mtazamo wake, Aya ya Kursi (Ayat al‑Kursi) ndiyo aya kuu na tukufu zaidi katika Qur’ani Tukufu, ingawa Qur’ani yote kwa ujumla ni neno la Mwenyezi Mungu.

Akizungumza katika kipindi cha televisheni kiitwacho “La‘allahum Ya‘qilun” (Huenda Wakafahamu) kinachorushwa na mtandao wa satelaiti wa DMC, Sheikh Al‑Jandi alieleza kuwa ibada haziko katika daraja moja, bali zinatofautiana kwa ubora na uzito wake, kwa mujibu wa gazeti la Al‑Masri Al‑Youm.

Aliongeza kuwa jukumu la Muumini si kufanya mema tu kwa ujumla, bali ni kujitahidi kufanya mema yaliyo bora zaidi na yenye uzuri mkubwa zaidi.

Sheikh Al‑Jandi alifafanua kwamba kuna dhana iliyoenea ambayo inahitaji kurekebishwa, nayo ni fikra kwamba kufanya mema kwa namna yoyote inatosha, ilhali kinachotakiwa ni kuchagua amali njema zilizo bora na zilizokamilika zaidi.

Akinukuu aya isemayo: “Na fuateni yaliyo bora zaidi katika yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu” (Surah Az‑Zumar, aya ya 55), alisisitiza kuwa mwongozo huu kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaonyesha kwamba hata ndani ya maandiko ya Qur’ani yenyewe kuna daraja na ubora unaotofautiana.

Al‑Jandi alisisitiza kwamba Qur’ani yote ni Neno la Mwenyezi Mungu na haina nafasi ya batili ndani yake, lakini baadhi ya aya zina hadhi ya juu zaidi kuliko nyingine.

Aliendelea kusema kwamba Aya ya Kursi ndiyo aya yenye hadhi ya juu zaidi katika Qur’ani Tukufu, ingawa aya zote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aya ya 255 katika Surah Al‑Baqarah ndiyo inayojulikana kama Aya ya Kursi (Ayat al‑Kursi).

3497347

Habari zinazohusiana
captcha