Kwa mujibu wa Shirika la Habari za Qur’ani la Kimataifa (IQNA), Dakta Larijani ameyasema hayo Jumanne katika ufunguzi wa mkutano wa tisa wa Umoja wa Mabunge ya nchi za Kiislamu mjini Tehran. Akihutubia katika kikao cha ufunguzi, Dakta Ali Larijani ambaye amepokea Uwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kiislamu kutoka kwa Spika wa Bunge la Sudan amesema kuwa, ulimwengu wa Kiislamu una nguvu ambazo zinaweza kutumiwa kukabiliana na ubeberu wa madola ya kikoloni. Spika wa Bunge la Iran ameashiria harakati za kikatili zinazofanywa na makundi yenye fikra finyu na mgando ya Kiwahabi na kusema: “Makundi hayo yanatumia mbinu za kikoloni za kutenganisha na kukufurisha Waislamu kwa shabaha ya kuharibu nishati na nguvu ya Umma wa Kiislamu na badala ya kufanya jitihada za kuimarisha umoja na mshikamano katika Umma na kutetea taifa linalodhulumiwa la Palestina yanawadhulumu Waislamu na kuhudumia malengo ya Wazayuni.
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kujadili kwa kina njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa kwa kina na wajumbe ni harakati za makundi ya takfiri ya Kiwahabi katika ulimwengu wa Kiislamu na kutafuta njia za kukabiliana na makundi hayo yanayoharibu sura halisi ya Uislamu.
Ajenda nyingine za mkutano huo ni kujadili hali ya mambo katika nchi za Kiislamu ikiwemo kadhia ya Palestina, umuhimu wa kustafidi na teknolojia ya kisasa ya nishati ya nyuklia kwa nchi zote na suala la kuweko mtazamo mmoja na mfungamano wa wanawake wa nchi za Kiislamu. Zaidi ya Maspika 30 na Manaibu 17 wa Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC pamoja na asasi 15 na jumuiya tazamaji za kigeni zinashiriki katika mkutano huo wa siku mbili unaofanyika hapa mjini Tehran.