IQNA

Qur'ani iliyoandikwa kwa hati za Imam Ali (as) yazua mjadala Yemen

19:20 - February 19, 2014
Habari ID: 1377495
Habari iliyochapishwa na gazeti la al Umanaa la Yemen kwamba rais wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh alitwaa na kuchukua nakala ya Qur'ani iliyoandikwa kwa hati za mkono inayonasibishwa kwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) imezusha mjadala mkubwa nchini humo.

Mwandishi wa Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) ameripoti kuwa, Imamu wa Msikiti wa Jamia wa Sanaa, Akram Ahmad al Ruqaihi amekadhibisha habari hiyo iliyochapishwa katika gazeti la al Umanaa. Amesema habari hiyo iliyochapishwa Jumatatu tarehe 17 Februari na kudai kuwa rais aliyeng'olewa madarakani wa Yemen Abdullah Saleh ametwaa nakala hiyo ya Qur'ani haina ukweli.
Imamu wa Msikiti wa Jamia wa Sanaa ameongeza kuwa, nakala hiyo ya Qur'ani Tukufu inahifadhiwa katika maktaba ya msikiti huo.
Awali gazeti la al Umanaa liliandika kuwa uongozi wa Msikiti wa Jamia wa  Sanaa ulimpa kiongozi wa zamani wa Yemen nakala hiyo inayonasibishwa kwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) inayojulikana kwa jina la Khatma ya Ali.
Uongozi wa Msikiti wa Jamia wa Sanaa umetangaza kuwa maktaba ya msikiti huo ambayo ina nakala muhimu na vitabu vilivyoandikwa kwa hati za mkono na vitabu nadra vya Kiislamu , mwezi Machi mwaka 2012 ilivamiwa na vitabu vyake kuibwa na watu wasiojulikana lakini nakala ya Qur'ani iliyoandikwa kwa hati za Imam Ali bin Abi Twalib (as) ilisalimika katika wizi huo. 1377069

Kishikizo: Qur'ani, imam Ali, yemen
captcha