Imearifiwa kuwa magaidi wa wanaojiita ‘Dola la Kiislamu Iraq na Sham’ kwa kifupi Daesh wametumia mabomu kubomoa msikiti huo Nabii Shayth AS ambaye anatambuliwa katika dini za Kiislamu, Kikristo na Kiyahudi kama mtoto wa tatu wa Nabii Adam na Hawa.
Aidha magaidi hao wamebomoa kaburi la Mtakatifu George katika mji huo wa Mosul. Kundi la Daesh liliuteka mji wa Mosul mwezi ulopita na kinara wao, Abu Bakr al Baghdadi ajakitangaza kuwa ‘khalifa’ wa eneo hilo. Afisa wa masuala ya turathi nchini Iraq Sami al-Massoudi amesema magaidi wa pote la Kiwahabi wa Daesh wanafuata itikadi inayoamini kuwa wanapaswa kumuua kila asiyeafikiana nao na kuongeza kuwa, itikadi wanayofuata haina uhusiano wowote na Uislamu. Hivi karibuni pia magaidi wa Daesh walibomoa kaburi la Nabii Yunus AS lililoko katika mji huo huo wa kale wa Mosul. Magaidi hao wa Daesh pia wamebomoa misikiti na maeneo kadhaa matakatifu ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Suni katika mkoa unaokumbwa na vita wa Nainawa nchini Iraq. Inaaminika kuwa magaidi wa Daesh wanapata uungaji mkono wa mashirika ya kijasusi ya Saudi Arabia na Qatar na pia himaya isiyo ya moja kwa moja ya utawala haramu wa Israel.