IQNA

Rais Hassan Rouhani

Kimya cha UNSC, chanzo cha jinai za Wazayuni

16:58 - August 04, 2014
Habari ID: 1435944
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuendelea kimya na kutojali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC ndio chanzo kikuu ambacho kimeufanya utawala wa Kizayuni wa Israel uendelee kupata kiburi cha kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran alipohutubu katika kikao cha Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) ambacho kimeandaliwa na Iran kwa lengo la kujadili kadhia ya Palestina na hasa yale yanayojiri katika Ukanda wa Ghaza. Rais  Rouhani ameelezea masikitiko yake  kuwa katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita na katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, utawala wa Kizayuni wa Israel umekiuka misingi yote ya ubinaadamu na sheria za kimataifa kwa kutumia silaha za maangamizi ya umati na zilizopigwa marufuku dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Ghaza. Ameongeza kuwa katika jinai hizo za kinyama, Israel imewaua mamia ya watoto kwa makusudi sambamba na kutekeleza mauaji ya umati. Rais wa Iran ameongeza kuwa utawala katili wa Israel pia umelenga maeneo ya kiraia kama vile shule, misikiti, miundo msingi na hata misafara ya wenye kutoa misaada.
Kikao hicho cha siku moja cha kamati ya Palestina ya mawaziri wa mambo ya nje wa NAM kinafanyika chini ya uenyekiti wa Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran. Kamati ya Palestina katika NAM inajumuisha Algeria, Bangladesh, Cuba, Iran, Misri, India, Senegal, Afrika Kusini, Zambia, Palestina, Zimbabwe, Indonesia na Malaysia. Wawakilishi wengine wa nchi za NAM pia wamehudhuria kikao hicho cha Tehran.
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kufanyika kikao hicho ni muhimu sana na ni ishara ya namna nchi za NAM zinavozingatia kwa kina kadhia ya Palestina. Rais Rouhani ameelezea matumaini yake kuwa NAM kama sehemu ya jamii ya kimataifa, ina uwezo mkubwa ambao unaweza kutumika kwa ajili ya kuwaletea Wapalestina waliodhulumiwa amani ya kweli na ya kudumu sambamba na kupata haki zao. Rais Rouhani ameitaka NAM ichukue hatua za haraka na za kivitendo za kusitisha jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza. Aidha amesema kwa kuzingatia kuwa Marekani inaunga mkono utawala dhalimu wa Israel, walimwengu hawana matumaini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

1435698

captcha