Makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa hapo jana ni ya siku 3 na yanalenga kutoa fursa kwa misaada ya kibinadamu kuwafikia watu wa Ghaza sambamba na kuruhusu kufanyika mazungumzo yenye lengo la kusitisha kabisa mapigano ambayo hadi sasa yamesababisha takriban Wapalestina 2000 kuuawa shahidi; wengi wao wakiwa raia wa kawaida hususan watoto wadogo na wanawake.
Jambo lenye kutoa mguso wa aina yake kuhusiana na makubaliano hayo ya usitishwaji vita ni jinsi vyombo vya habari vya ndani na nje ya utawala haramu wa Israel vinavyoendelea kuakisi kwa upana kufeli Tel Aviv kufikia malengo yake haramu kwenye vita hivyo vya takriban mwezi mzima. Kuhusiana na muktadha huo, gazeti la kila siku la Yedi'ot Aharonot linalochapishwa Tel Aviv limeandika makala ndefu inayoeleza jinsi Israel ilivyofeli kwenye vita vya Ghaza na mafanikio waliopata wanamapambano wa Kipalestina. Jambo hilo pia limekuwa likizungumzwa na viongozi waandamizi wa utawala wa Kizayuni japo nyuma ya pazia.
Miongoni mwa nukta za wazi zinazoonyesha kweli Israel imevurunda kwenye mahesabu yake huko Ghaza ni kukubali utawala huo kutekeleza masharti ya makundi ya muqawama ya Palestina ya kuondoa majeshi yake kwenye ukanda huo kabla ya kufikiwa aina yoyote ya makubaliano ya usitishwaji vita. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, punde baada ya kufikiwa makubaliano ya muda ya usitishaji vita kwa masaa 72 kati ya Israel na wanamapambano wa Palestina, utawala bandia wa Israel ulianza mara moja kuondosha majeshi yake huko Ghaza na kuyapeleka katika eneo la mpakani.
Baadhi ya duru zinaripoti kwamba, Israel pia imekubali shingo upande kwamba, kwenye makubaliano ya muda mrefu iko tayari kutekeleza masharti mengine ya wanamuqawama wa Palestina ikiwa ni pamoja na kuondoa mzingiro wa Ghaza pamoja na kuwaachia huru wafungwa wa Kipalestina. Huko nyuma utawala wa Kizayuni mara kadhaa ulisaini makubaliano ya usitishaji vita lakini ukavunja makubaliano hayo muda mfupi baada ya kuanza kutekelezwa. Kukubali utawala huo ghasibu kutekeleza kikamilifu makubaliano ya hivi punde tena chini ya masharti ya wanamapambano wa Palestina unaonyesha jinsi muqawama ulivyopata nguvu na ushindi katika vita hivyo ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Wachambuzi wengi wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni, kwa kushindwa kufikia malengo yake katika vita vyake vya mwezi mzima huko Ghaza, imepata pigo kubwa kijeshi na kisiasa sambamba na kuzidisha hasira na chuki za walimwengu dhidi yake kutokana na mauaji ya kinyama uliyofanya dhidi ya watoto na wanawake wasio na hatia.