Ripoti iliyotolewa na maulama hao na kusomwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya Maulama na mkuu wa zamani wa wanazuoni wa chuo kikuu hicho cha al-Azhar, Ahmad Omar Hashim, imesema kuwa, ni haramu kufukua au kugusa mabaki ya mwili wa Mtukufu Mtume (saw). Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria, Mitume wa Mwenyezi Mungu huzikwa mahala walipofia na kwamba kaburi la Mtume lipo hapo na litaendelea kuwa hapo daima. Hisham amesema kuwa, haifai kukabiliana na vyanzo muhimu vya sheria ambavyo ni aya za Qur'ani na Hadithi na kwa sababu hiyo haifai kutelekeza mpango huo kwa hoja eti ya upanuzi wa Msikiti wa Madina au sababu nyengineyo.
Msomi mmoja wa Saudi Arabia alikuwa ametoa pendekezo la kubomolewa kaburi la Mtume (saw) na mabaki yake kuzikwa upya kwa siri katika makaburi ya Baqii, ikiwa ni pamoja na kuharibiwa vyumba vilivyokuwa vikitumiwa na Watu wa Nyumba ya Mtume (s.a.w) yaani Ahlul Bayt (a.s) sambamba na kuvunjwa Kuba la Kijani ambalo ndilo nembo ya msikiti wa Mtume (s.a.w). habari zinasema pendekezo hilo limekwishawasilishwa kwa wakuu wa msikiti huo mjini Madina na kwamba bado hakujachukuliwa uamuzi wowote.
Baraza Kuu la Maulama wa al-Azhar limelitaja pendekezo hilo kuwa limefeli na kuonya kwamba, iwapo mpango huo utatekelezwa, utazusha fitina kubwa katika Umma wa Kiislamu na kwamba unalenga kuwaingiza Waislamu katika mgogoro ambao haijulikani hatima yake.