Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya nchi za Kiafrika na Kiarabu Hussein Amir Abdullahiyan amesema kuwa, matamshi yaliyotolewa na Saud al Feisal Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia dhidi ya Iran yanakinzana kikamilifu na mazingira ya hivi sasa ya kufanyika mazungumzo ya kidiplomasia ya pande mbili. Abdullahiyan ameitanabaisha serikali ya Riyadh kuwa macho na njama za maadui wa eneo la Mashariki ya Kati. Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ameongeza kuwa, Iran ni nchi iliyopiga hatua kubwa zaidi kwenye mapambano dhidi ya ugaidi na kusisitiza kwamba, Tehran itaendelea kuzisaidia serikali na wananchi wa Iraq na Syria katika mapambano dhidi ya magaidi katika kalibu ya sheria za kimataifa. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Saudi Arabia jana alitoa matamshi ya kiburi dhidi ya Iran kwa kudai kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni sehemu ya matatizo yaliyoko Syria. Saud al Feisal ametoa madai hayo katika hali ambayo, kuna maelfu ya raia wa Saudi Arabia wanaopigana bega kwa bega na makundi ya kigaidi katika nchi za Syria na Iraq. Tuhuma za Saud al Feisal zinatolewa katika hali ambayo, hivi karibuni serikali ya Saudi Arabia kwa kushirikiana na Marekani ziliweka kambi ya kijeshi nchini Saudia, kwa lengo la kutoa mafunzo kwa makundi ya kigaidi yanayopelekwa nchini Syria.../mh