Shirika la habari la Iqna limenukuu habari ya shirika la habari la Ufaransa (AFP) kwamba Wizara ya Habari ya Morocco imetoa taarifa ikipiga marufuku ugawaji wa toleo la hivi karibuni la jarida la L'Express Internatonal kwa sababu ya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuchapishwa kwa picha iliyokuwa juu ya jarida hilo ambayo chini yake kuna maandishi yanayosema: "Mgongano, ujumbe, mwenendo na mtazamo wa Muhammad na Masihi" ndiyo sababu kuu ya kupigwa marufuku jarida hilo.
Uamuzi huo umechukuliwa kwa mujibu wa kipengee cha 29 cha katiba ya Morocco. Kipengee hicho kinaipa Wizara ya Habari haki ya kuzuia uchapishwaji wa majarida ya kigeni yanayovunjia heshima dini ya Kiislamu, serikali ya Morocco na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
Jarida hilo limetolewa kwa mnasaba wa mkutano wa viongozi wa Kikristo na Kiislamu uliopangwa kufanyika tarehe nne mwezi huu wa Novemba katika mji mkuu wa Italia, Roma. Kati ya makala sita zilizochapishwa kwenye jarida hilo ambazo kimsingi zinazungumzia tofauti kati ya Ukristo na Uislamu, kuna makala yenye kicha cha habari kisemacho: "Masihi, Ujumbe wa Uasi, na nyingine inayosema: Muhammad, Mtume na Mpenda vita."
Mhariri Mkuu wa jarida hilo la Kifaransa Christian Makarian ambaye pia ni mwandishi wa kitabu cha "Mgongano wa Muhammad na Masiya" amedai kuwa hajui sababu ya jarida hilo kupigwa marufuku na kwamba sura ya Mtume Muhammad SAW katika picha iliyochapishwa juu ya jarida hiyo haikudhihirishwa kama ishara ya kuheshimu itikadi za Waislamu wa Morocco!
Inatazamiwa kuwa jarida hilo vilevile litapigwa marufuku kuingizwa katika nchi za Tunisia na Aljeria kwa sababu hiyo hiyo ya kuyavunjia heshima matukufua ya Kiislamu. 313776