Naibu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiislamu ya Italia Yahya Palavichini amesema kuwa mkutano huo ni fursa ya kuimarisha mazungumzo kati ya wanafikra wa Kiislamu na wawakilishi wa kanisa Katoliki na kujenga maelewano zaidi kati ya wafuasi wa dini za Kiislamu na Kikristo.
Palavichini amesema kuwa, miongoni mwa ajenda za mkutano huo ni kufungua mlango wa mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo, kusisitiza juu ya udharura wa kuheshimiwa hadhi ya mwanadamu kote duniani, wito wa urafiki na udugu kwa msingi wa imani ya Mungu Mmoja, kutafuta njia bora za kutambua na kuondoa hitilafu za kimitazamo kati ya wafuasi wa dini za Uislamu na Ukristo, na kutoa fursa ya wafusi wa dini hizo kutambua misingi ya mafundisho ya dini za mbinguni.
Ameashiria kwamba, wanazuoni wa Kiislamu wanaoshiriki katika mkutano huo wanajumuisha wasomi wa Kishia na Kisuni na kuongeza kuwa mkutano huo unafanyika katika fremu ya mpango wa mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo uliopewa jina la mpango wa "Neno Sawa" uliotiwa saini na wanafikra 138 wa Kiislamu na viongozi kadhaa wa makanisa kote duniani.
Naibu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiislamu ya Italia amesema, wanafikra wa Kiislamu wanaoshiriki kwenye mkutano huo wa siku tatu wana matumaini ya kufikia msimamo wa pamoja kuhusu ufumbuzi wa migogoro na mivutano iliyopo kati ya Uislamu na Ukristo katika mazungumzo yao na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Dunia Papa Benidict wa 16 na viongozi wa makanisa. 315570