Sheikh Abul Einein Sheisha, msomaji mashuhuri wa Qur'ani mzali wa wa Misri, ameteuliwa kuwa balozi wa usomaji Qur'ani katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na mahudhurio yake makubwa katika hafla na vikao mbalimbali vya Qur'ani.
Hii ni kwa sababu amekuwa akiacha kumbukumbu kubwa na muhimu ya usomaji Qur'ani kila mara anapohudhuria katika vikao kama hivyo vya usomaji kitabu hicho kitakatifu cha Mwenyezi Mungu.
Abul Ainein Sheisha ni miongoni mwa wasomaji mashuhuri wa Qur'ani katika ulimwengu wa Kiislamu ambaye ametumia umri wake wote katika njia hiyo, na nyadhifa nyingi za Qur'ani ambazo amezihudumia katika uwanja huo ni ushahidi tosha wa kuthibitisha jambo hilo. Sheisha ameteuliwa kuhudumu katika nyadhifa hizo zote kutokana na ujuzi na uzoefu wake mkubwa kuhusiana na masuala ya Qur'ani. Moja ya nyadhifa hizo ni kuchaguliwa kuwa msomaji rasmi wa Qur'ani katika Msikiti wa Bibi Zeinab (AS) nchini Misri. Hivi sasa Sheisha anahudumu kama mkuu wa Umoja wa Wasomaji Qur'ani wa Misri, mwanachama wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Misri, mwanachama wa Kamati Kuu ya Qur'ani inayofungamana na Wizara ya Wakfu ya Misri, mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Cairo na mwanachama wa Kamati ya Ujenzi wa Misikiti ya mji huo. Moja ya sifa za pekee za Sheisha ni kuwa ni msomaji wa kwanza wa Qur'ani wa Misri kusoma kitabu hicho kitakatifu katika Msikiti Mtukufu wa al-Aqswa. Sheikh Sheisha pia amekuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha Waislamu wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu kupitia usomaji wake wa Qur'ani katika vikao mbalimbali vya Qur'ani. 316507