IQNA – Ilimchukua mwaka mmoja tu tangu kuifahamu dini ya Uislamu hadi kufika katika Msikiti Mkuu wa Makkah (Masjid al-Haram), akishiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur’ani Tukufu.
Kisa cha mshiriki kutoka Burundi, Pentra Bushima Amin, kilianza alipokuwa na umri wa miaka 14, baada ya rafiki yake Mwislamu kumwalika kujifunza kuhusu Uislamu na kumtambulisha kwa maadili, tabia njema na fadhila za dini hiyo.
Mafundisho ya Uislamu yalimgusa sana, na akaamua kuingia katika Uislamu. Uamuzi huo ulishuhudiwa na familia yake, ambapo watu wanne wa familia hiyo, akiwemo wazazi wake na dada yake, pia walisilimu pamoja naye.
Baada ya kusilimu, Pentra hakuchukua muda kuanza safari yake ya kujifunza Qur’ani Tukufu. Alianza kuihifadhi kwa azma kubwa na shauku ya dhati ya kujifunza, na akafanikiwa kuhifadhi Qur’ani yote ndani ya miezi mitano tu.
Baadaye aliendelea kufanya marudio na kuimarisha hifdhi yake hadi akaihifadhi Qur’ani Tukufu kikamilifu.
Kuhifadhi Qur’ani hakukuwa mwisho wa safari yake, bali ulikuwa mwanzo wa ukurasa mpya wa mafanikio. Baadaye alishiriki katika mashindano ya ndani nchini Burundi yaliyowakutanisha takribani washiriki 500, na kushika nafasi ya kwanza.
Kutokana na ushindi huo, alichaguliwa kuiwakilisha nchi yake katika Mashindano ya Kimataifa ya Mfalme Abdulaziz ya Kuhifadhi, Kusoma na Kufasiri Qur’ani Tukufu. Miezi michache baadaye, alijikuta katika Msikiti Mkuu wa Makkah akiwa pamoja na wahifadhi wa Qur’ani kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Leo, Pentra yuko katika Msikiti Mkuu wa Makkah, akiiwakilisha Burundi katika Mashindano ya 46 ya Kimataifa ya Mfalme Abdulaziz ya Kuhifadhi, Kusoma na Kufasiri Qur’ani Tukufu, pamoja na washiriki 334 wa kiume na wa kike kutoka nchi 133.
3498632