IQNA – Shule ya Qur’ani ya ‘Gaza’ iliyoko katika mkoa wa Hama Bouziane, jimbo la Constantine nchini Algeria, imejitolea kwa miaka 24 kufundisha na kuwezesha kuhifadhi Qur’ani Tukufu. Taasisi hii imekuwa mwanga wa maarifa na malezi ya kiroho, ikitoa mafunzo kwa mamia ya wahifadhi wa kiume na wa kike.
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya Al-Nasr, mamia ya wazazi nchini Algeria, wakiepuka vishawishi vya mitaani na skrini za kielektroniki, huwaandikisha watoto wao katika shule za Qur’ani kila msimu wa kiangazi. Hii ni kutokana na imani thabiti katika thamani ya taasisi hizi kwa ajili ya matumizi bora ya wakati na kuimarisha maadili ya kidini. Shule ya Qur’ani ya ‘Gaza’ inang’ara zaidi katika muktadha huu; kwa zaidi ya miongo miwili, imekuwa kimbilio la elimu na malezi bora.
Shule na Msikiti
Historia ya shule hii inashabihiana na historia ya mahali ilipo. Shule hiyo ilijengwa juu ya magofu ya msikiti wa zamani wa Hassanein, eneo ambalo wakati wa ukoloni wa Kifaransa lilikuwa chumba cha utesaji, ardhi ambayo ilikuwa imezaporwa kutoka kwa waumini wa eneo hilo, lakini baada ya uhuru, ilirejeshwa katika utumishi wa Allah.
Baada ya ujenzi wa msikiti mpya wa Hassanein mnamo 1986, wazo la kuanzisha shule huru ya Qur’ani kwa ajili ya kizazi kipya liliibuka. Tangu kufunguliwa kwake, shule imekuwa ikitekeleza wajibu wake wa kielimu, ikivutia wanafunzi kutoka Hama Bouziane na maeneo mengine ya Constantine. Shule inatoa programu za kielimu zinazoendana na rika mbalimbali, ikiwemo madarasa ya awali kwa watoto, mafunzo ya kusoma na kuandika kwa watu wazima, na programu maalum ya utoaji wa idhini ya Qur’ani (ijazah).
Kulea vizazi kwa misingi ya Kiislamu
Mkuu wa shule, Muhammad Taher Murad, alisisitiza kuwa shule hii si nafasi ya kuhifadhi Qur’ani pekee, bali ni kituo cha kulea vizazi kwa misingi ya maadili ya Kiislamu. Alieleza kuwa mwitikio mkubwa wa kozi za kiangazi unaonyesha imani ya wazazi katika jukumu la shule hii.
Murad alibainisha kuwa ingawa shule inafanya kazi mwaka mzima, shughuli zake huongezeka wakati wa likizo. Katika kozi ya hivi karibuni ya kiangazi, wanafunzi 433 walisajiliwa katika vikundi 18 chini ya usimamizi wa walimu wanawake waliobobea katika elimu ya Qur’ani. Hii ni jaribali makini na la kimkakati la kulinda utambulisho wa kiislamu dhidi ya mmomonyoko wa maadili.
Programu Maalum ya Kusoma na Kuandika
Samah Daouadi, mwalimu wa Qur’ani shuleni hapo, alieleza kuwa taasisi hiyo haijajikita kwa watoto pekee; pia inawakaribisha watu wazima, ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, akina mama wa nyumbani, na wanawake, kupitia programu maalum iliyoundwa ili kuhifadhi sehemu za Kitabu cha Allah.
3498649