IQNA

Haddad Adel ateuliwa kuwa msomi wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu

9:10 - November 09, 2008
Habari ID: 1705976
Haddad Adel, Mkuu wa Kamisheni ya Masuala ya Utamaduni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameteuliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kihistoria, Sanaa na Utamaduni ya Umoja wa Nchi za Kiislamu IRCICA kuwa msomi na shakhsia wa masuala ya kiutamaduni wa Ulimwengu wa Kiislamu.
Uteuzi huo unatokana na juhudi zake kubwa katika uandishi na utafiti kuhusiana na masuala ya Kiislamu. Kwa mujibu wa Ikna hiyo ni mara ya kwanza kwa raia wa Iran kuchaguliwa kuwa shakhsia wa kiutamaduni kati ya shakhsia kama hao wa nchi 57 wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiislamu OIC. Hii ndio maana umoja huo ukaamua kumfanyia shererhe shakhsia huyo pamoja na kumpa zawadi maalumu kama alama ya shukrani zake kwake kutokana na juhudi kubwa za utafiti ambazo amezifanya katika ulimwengu wa Kiislamu. Umoja wa Nchi za Kiislamu huchagua na kufanya sherehe kama hizo kila baada ya miaka mitano kwa ajili ya kuwaenzi shakhsia wa kiutamaduni wa nchi wanachama. Baada ya kupokea zawadi hiyo, Haddad Adel alisema katika hotuba aliyotoa katika sherehe hizo kwamba, Uislamu una ustaarabu mkubwa na muhimu zaidi katika historia ya mwanadamu na kuongeza kuwa, wanazuoni wa Kiislamu wana jukumu muhimu katika kuimarisha na kueneza fikra ya elimu na utamaduni duniani. Haddad Adel amesema kwamba, tunaishi katika ulimwengu ambao mwanadamu anahitajia imani na maadili kuliko wakati mwingine wowote na kwamba Waislamu wanapasa kuzingatia utambulisho wao wa kimaanawi na kijamii ili kuweza kufidia kubaki kwao nyuma kupitia juhudi na jitihada. Haddad Adel ametoa pendekezo la kuundwa kundi la wasomi na wanafikra wa Kiislamu ambao wanafahamu vyema mahitaji ya zama hizi ya ulimwengu wa Kiislamu na mazingira ya kustawishwa elimu katika jamii za Kiislamu, ili kwa njia hiyo watoto na vijana wanaoinukia waweze kuhamasishwa kufuatilia masuala ya kielimu. 317037
captcha