Katika hali ambayo ulimwengu wa Kiislamu unafanya jitihada kubwa za kuzima njama za Wamagharibi kwa kuwaunganisha na kukutanisha Waislamu wote chini ya mwavuli wa umoja, Mawahabi 190 wenye misimamo mikali wa Saudi Arabia wametoa taarifa wakidai kwamba Waislamu wa Shia Ithnaashari na Suni wanahitilafiana katika misingi ya kiitikadi mbali na masuala madogo ya kifiqhi.
Taarifa hiyo ambayo imechapishwa kwenye mtandao mmoja wa intaneti wa Mawahabi wenye misimamo mikali, imesema kuwa, iwapo ubaguzi wa kimadhehebu unaofanywa dhidi ya raia Mashia katika nchi za Saudi Arabia na nchi nyingine za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi utafutwa, suala hilo litatayarisha uwanja mzuri wa kueneza zaidi madhhebu ya Shia kati ya Waislamu wa Kisuni!
Watu waliotia saini taarifa hiyo wametoa madai ya urongo wakisisitiza juu ya hatari eti ya Shia ambao wamesema, wana rasilimali kubwa kwa ajili ya kueneza madhehebu hiyo katika jamii za Wasuni.
Wanafikra hao wa Kiwahabi wa Saudi Arabia wamedai kwamba mashia wanayalinganisha matamshi na semi za Maimamu wao na hadithi za Mtume na kwamba maulama wa Kishia wanapaswa kutazama upya vitabu vyao katika uwanja huo.
Katika upande mwingine mwanazuoni wa Kishia wa Saudi Arabia Hassan al Safar mapema mwezi huu alihutubia mkutano wa wanafikra wa eneo la Qatif huko magharibi mwa Saudi Arabia akieleza wasiwasi wake kuhusu hatua dhaifu za serikali ya Riyadh katika kutatua masuala yanayohusiana na ubaguzi wa kimadhehebu. 317663