IQNA

Kuanza kwa duru ya pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanafunzi Waislamu wa Vyuo Vikuu.

10:33 - November 11, 2008
Habari ID: 1706939
Duru ya pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Wanafunzi Waislamu wa Vyuo Vikuu yalianza jana usiku mjini Tehran yakihudhuriwa na Mkuu wa Vyombo vya Sheria nchini Iran Ayatullah Mahmoud Shahrudi na Meya wa jiji la Tehran Dr. Muhammad Baqir Qalibaf.
Mashindano hayo yanafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Kimataifa cha Milad.
Ayatullah Mahmoud Shahrudi alihutubia kikao hicho cha ufunguzi akisema kuwa kama Qur’ani isingekuwepo ingekuwa muhali kwa mwanadamu kuwasiliana na Mola Muumba na kwamba ni kupitia Nabii Muhammad SAW ndipo mwanadamu aliweza kufikia daraja ya kuwasiliana moja kwa moja na ulimwengu wa ghaibu na kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Shahrudi amesema, Qur’ani ni chemchemi ya nuru na uongofu wa mwanadamu na akaongeza kuwa, Mwenyezi Mungu SW aliweka vyanzo vya mahitaji yote ya mwanadamu na funguo za saada na ufanisi wake katika awamu zote za maisha ndani ya kitabu cha Qur’ani. Amesema, hiyo ndiyo njia nyoofu ambayo Mwenyezi Mungu alimfungulia mwanadamu kupitia Mitume wake. Amesisitiza juu ya udharura wa kufahamu vema njia ya uongofu wa mwandamu ambayo ni Qur’ani na Ahlubaiti wa Mtume Muhammad SAW.
Kikao cha ufunguzi wa Mashindano ya Kimataifa ya Wanafunzi Waislamu wa Vyuo Vikuu kilihutubiwa pia na Meya wa jiji la Tehran Muhammad Baqir Qalibaf, Mwenyekiti wa mashindano hayo Rahim Khaki, Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Abbas Sadri na wanafikra na wasomi wengine kadhaa kutoka nchi mbalimbali.
Jopo la majaji wa mashindano hayo ya kimataifa la wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka nchi 40 duniani linaongozwa na msomaji mkongwe na mashuhuri wa Qur’ani kutoka Misri Abul Einein Sheisha. 318700

captcha