IQNA –Mwongozo mpya wa kanuni za Mashindano ya Kimataifa ya 46 ya Mfalme Abdulaziz ya Kuhifadhi, Kusoma, na Kufasiri Qur’ani Tukufu umezinduliwa rasmi.
Waziri wa Masuala ya Kiislamu, Da’wah na Mwongozo wa Saudi Arabia, ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mashindano ya Ndani na ya Kimataifa ya Qur’ani, Abdullatif Al Alsheikh, amezindua hatua hiyo mpya ya mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 Safar hadi tarehe 6 Rabi’ al-Awwal 1448 Hijria.
Msimu huu umeweka rekodi mpya kwa kushirikisha jumla ya washindani 334, wakiwemo wanaume na wanawake, kutoka nchi 133 duniani, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi ya washiriki kuwahi kurekodiwa tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.
Mashindano haya yanalenga kuwahimiza Waislamu, wanaume kwa wanawake, kujishughulisha kikamilifu na Qur’ani Tukufu kupitia kuhifadhi, kufahamu, na kuzingatia aya zake; kukuza roho ya ushindani wa kiadilifu na wenye afya miongoni mwa mahafidh wa Qur’ani; pamoja na kuimarisha uhusiano na mafungamano ya vijana na Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu.
Katika kuonyesha maendeleo endelevu ya mashindano hayo, msimu huu umerekodi kiwango kikubwa zaidi cha zawadi tangu kuanzishwa kwake, kikifikia jumla ya Riyal za Saudi (SAR) 10,260,000.
3498452