IQNA

Idhaa ya Redio ya Qur’ani Tukufu ya Oman yaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake

17:21 - July 29, 2026
Habari ID: 3482556
i
IQNA – Idhaa ya Qur’ani Tukufu ya Usultani wa Oman imeadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanza kurusha matangazo yake siku ya Jumatatu.

Idhaa hii imejitolea maalum kwa ajili ya Qur’ani Tukufu na sayansi zake, ambapo hurusha visomo vya Qur’ani kwa qira’at na riwaya mbalimbali vilivyosomwa na wasomaji wa rika tofauti na wa jinsia zote mbili, sambamba na kuwasilisha vipindi maalum vyenye malengo na maudhui ya kitaalamu kuhusu Kitabu cha Mwenyezi Mungu na sayansi zake.

Idhaa ya Redio ya Qur’ani Tukufu ilianza matangazo yake ya majaribio kwa saa saba kila siku mnamo mwaka 2006, kabla ya kupanua matangazo hayo na kuwa ya saa 24 mfululizo kuanzia tarehe 1 Januari 2014, kupitia vituo 28 vya urushaji matangazo vinavyofunika mikoa mbalimbali ya Oman, pamoja na matangazo ya satelaiti na mtandao wa “Ayn”, hali inayowezesha wasikilizaji kufuatilia matangazo hayo ndani na nje ya nchi.

Redio hii inaendesha shughuli zake kwa mujibu wa dira madhubuti inayojikita katika kuimarisha misingi ya wastani (kujiepusha na itikadi kali), usawa, na uvumilivu katika Uislamu, maadili ambayo yanapamba jamii ya Oman, huku ikiongozwa na misingi ya Kiislamu inayolingania maelewano na kusogeza karibu madhehebu mbalimbali ya Kiislamu na kukuza umoja, udugu, na huruma miongoni mwa wanadamu.

Ndugu Ahmed bin Muhana al-Kindi, Mkurugenzi wa Idara ya Idhaa ya Qur’ani Tukufu katika Kurugenzi Kuu ya Redio chini ya Wizara ya Habari, alieleza kuwa kupita kwa miaka 20 tangu kuanzishwa kwa idhaa hii nchini Oman ni hatua muhimu sana katika safari yake ya kihabari. Tangu kuanzishwa kwake, idhaa hiyo imekuwa na shauku kubwa ya kuwa jukwaa la kueneza Qur’ani Tukufu, kuimarisha maadili mema ya Uislamu yanayohimiza wastani na maelewano, na kutoa maudhui yenye nguvu ya kielimu na ki-Qur’ani yanayokidhi mahitaji ya tabaka mbalimbali za jamii.

Aliongeza kuwa katika safari hii, redio hiyo imeshuhudia maendeleo endelevu katika saa za matangazo na ubora wa maudhui, ikihamia kwenye matangazo ya saa 24 na kutoa visomo vya Qur’ani kwa riwaya tofauti, pamoja na vipindi maalum vya sayansi za Qur’ani Tukufu, tafsiri, sheria za tajwidi, na maadili ya Kiislamu, ikitumia njia mbalimbali za kisasa za mawasiliano ili kuwafikia wasikilizaji ndani na nje ya nchi.

Kuhusu visomo vya Qur’ani (tilaawah), alibainisha kuwa maktaba ya Idhaa hiyo inajumuisha rekodi za Qur’ani zilizosomwa na maqari mashuhuri kutoka kote katika Ulimwengu wa Kiislamu. Pia inajumuisha rekodi kamili za Qur’ani katika riwaya mbalimbali ambazo hurushwa kipekee na idhaa hiyo, zikiambatana na vipindi maalum vinavyozifafanua riwaya hizo. Aidha, redio hiyo imerekodi Qur’ani nzima zilizosomwa na maqari wa Oman, pamoja na visomo vingine vilivyorekodiwa na wasomaji hao kwa riwaya ya Hafs kutoka kwa Asim na riwaya ya Qalun.

Kuhusu kuwawezesha wasomaji wa ndani wa Oman, alieleza kuwa redio hiyo imetoa kipaumbele kikubwa kurekodi Qur’ani nzima zilizosomwa na maqari wa Oman kutoka mikoa mbalimbali na wa umri tofauti.

Pia iliwapa nafasi maqari wa Oman kufanya kazi ya kusahihisha na kukagua visomo wakati wa kurekodi na baada ya kukamilika, akibainisha kuwa Kamati ya Kuchagua Maqari katika Redio na Televisheni inajumuisha jopo la maprofesa waliobobea katika sayansi ya qira’at na visomo vya Qur’ani.

Alifafanua kuwa Idhaa ya  Qur’ani Tukufu ilipata alama za juu zaidi za kuridhisha katika kura ya maoni ya wananchi kuhusu kuridhishwa na vipindi vya Idhaa na Televisheni ya Usultani wa Oman, iliyofanywa na Kituo cha Kitaifa cha Takwimu na Taarifa mnamo mwaka 2025.

Zaidi ya hayo, vipindi kadhaa vilivyotangazwa na idhaa hiyo vimeshinda tuzo mbalimbali katika eneo la Ghuba ya Uajemi na ulimwengu wa Kiarabu, vikiwemo “Deen Al Rahmah” (Dini ya Rehema), “Atheer Al Arabiyyah” (Anga la Lugha ya Kiarabu), na “Qiyamuna Hawiyyatuna” (Maadili Yetu ndio Utambulisho Wetu).

Amesema kuwa idadi ya vipindi vinavyowasilishwa na redio hiyo katika ratiba ya sasa imeongezeka na kufikia zaidi ya vipindi 22, ikilinganishwa na vipindi 8 pekee katika msimu wa kwanza wa matangazo mnamo mwaka 2006.

3498443

captcha