IQNA

Mwandishi wa Hati wa Yemen anayehafidhi urithi asili wa uandishi wa Qur’ani Tukufu

17:11 - July 28, 2026
Habari ID: 3482548
IQNA – Ali Qassem ni mwandishi wa hati (khatati au kaligrafia) kutoka nchini Yemen ambaye amejitolea katika kuhifadhi mapokeo ya kale ya uandishi wa Qur’ani Tukufu kwa kutumia hati ya Kiuthmaniya (Rasm al-Uthmani).

Kwa mujibu wa ripoti ya televisheni ya Al-Araby, amekuwa akifuatilia lengo hili kwa mapenzi makubwa na shauku ya kipekee inayodhihirisha mapenzi yake ya dhati kwa Neno la Allah (SWT.).

Ndugu Qassem anaendeleza mapokeo haya ya kale ya uandishi wa hati za Qur’ani kwa kuandika aya za Mwenyezi Mungu kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia sheria na kanuni thabiti za uandishi wa Kiuthmaniya. Sanaa hii, kwa mujibu wake, chimbuko lake kuu ni kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na juhudi za kuulinda urithi asili wa Kiislamu.

Qassem, ambaye anafanya kazi zake katika karakana ndogo iliyopo nyumbani kwake mjini Sana’a, huchovya kalamu yake kwenye wino kwa tahadhari kubwa kabla ya kuandika kila herufi, akichanganya shauku yake binafsi na sanaa hii ya kimapokeo yenye kanuni madhubuti na maalum.

Khatati huyu wa Yemen anaeleza kuwa, mchakato wa uandishi wa aya za Qur’ani Tukufu unatofautiana kabisa na uandishi wa matini nyingine yoyote ile.

Ameonesha mfano wa kazi yake ya kwanza aliyoiandika kwa kutumia hati ya Naskh, ambayo ndiyo hati inayotumiwa zaidi katika uandishi wa Qur’ani, kisha akafafanua kuhusu uandishi wa Qur’ani kwa kutegemea hati ya Kiuthmaniya. Amesema kuwa aina hii ya uandishi inasimama juu ya sheria sahihi na thabiti zinazozingatia kwa namna ya pekee maana, ufasaha wa lugha (balagha), na tafsiri ya Qur’ani Tukufu.

Kuhusu karatasi zinazotumiwa katika uandishi wa hati za Qur’ani, Qassem ameeleza kuwa huko nyuma zilitumika karatasi maalum za kienyeji, lakini hivi sasa zinatumika karatasi za kisasa za viwandani ambazo humwezesha mwandishi kufanya sanaa hii bila wino kuvuja au kupenya upande wa pili wa karatasi na kuacha alama.

Kuhusu motisha katika kuendelea na njia hii, msanii huyu wa Yemen amesema: “Motisha yangu ya kwanza kabisa ni mapenzi na mfungamano wangu na Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Pili, uandishi wa Qur’ani Tukufu ni heshima kubwa na amana nzito, na tatu, kazi hii inanipa fursa ya kukuza na kuimarisha kipaji changu katika sanaa ya uandishi wa hati.”

Amesisitiza kwa kusema: “Tangu nilipoingia katika uwanja wa uandishi wa hati, hakuna kitu kilichonisaidia kukuza kipaji hiki kama uandishi wa Qur’ani Tukufu.”

3498439

captcha