Mogens S. Mogensen, Mwandishi wa Denmark aliyeandika kitabu kiitwacho ‘Tokea Mgogoro wa Vikatuni hadi Hijabu’ ameituhumu serikali ya nchi hiyo kuwa inaunga mkono na kutetea gazeti la Jyllands-Posten lililochapisha hivi karibuni picha na vikatuni vinavyokejeli na kumkosea adabu Mtume Muhammad (saw).
Mwandishi wa kitabu hicho amechunguza kwa urefu mgogoro uliozuka ulimwenguni kufuatia kuchapishwa vikatuni hivyo vya dharau na matusi dhidi ya Mtume Mtukufu (saw) mwaka 2005 na athari za mgogoro huo katika ngazi za kimataifa na ndani ya Denmark yenyewe. Mwandishi amesema katika kitabu chake kwamba, serikali ya Denmark imetumia vibaya sheria ya kupambana na ugaidi na kwamba kupitia uungaji mkono wa chama chenye misimamo ya kupindukia cha Wananchi, imekuwa ikiwaudhi na kuwasumbua Waislamu kwa kuwatia nguvuni na kuwasaili, bila ya kuwepo sababu yoyote ya kimsingi. Mwandishi huyo amesema kuwa matamshi ya chuki na uchochezi ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi wa Denmark dhidi ya Waislamu na kuchapishwa kwa picha na vikatuni dhidi ya Mtume tarehe 30 Septemba mwaka 2005, haikuwa hatua iliyotokea hivi hivi bali ni jambo lililopangwa kwa utaratibu maalumu na makundi yenye chuki dhidi ya Uislamu ya Denmark. 317740