Sayyid Thamar ad-Deen Swamdaf, msomaji Qur’ani kutoka katika nchi ya Tajikistan ametoa pendekezo la kuongezwa uwanja wa kitaaluma wa ‘maana’ na ‘tafsiri’ katika nyanja za mashindano ya kimataifa ya wanachuo wa nchi za Kiislamu katika miaka ijayo.
Swamdaf ambaye ameshiriki katika duru ya pili ya mashindano hayo yanayofanyika nchini Iran ametoa pia pendekezo la kushirikishwa wanachuo wa kike katika mashindano hayo akisema kuwa jambo hilo litawashawishi kuizingatia zaidi Qur’ani na kuwapa moyo wa kushindana na wanafunzi wenzao wa kume katika jambo hilo la kheri. Amesema, sauti ya msomaji Qur’ani ina athari kubwa katika kumfanya msikilizaji azingatie maana ya kitabu hiki kitakatifu na kwamba msomaji anapasa kusoma kwa sauti nzuri na ya kuvutia huku akizingatia sheria na kanuni zote za usomaji wa aya za Qur’ani hasa anaposoma aya zinazohusiana na Pepo na moto wa Jahannam. Amesema, katika hatua ya mwanzo, kwanza msomaji wa Qur’ani mwenyewe anapasa kuwa mtu mwema anayefuata mafundisho yote ya kitabu hicho kitakatifu kwa sababu Qur’ani si kitabu cha kusomwa tu bali ni kitabu cha matendo na amali njema. Ameongeza kuwa utekelezaji wa mafundisho ya kitabu hicho cha mbinguni unaweza kuwa muongozi muhimu na wa kimsingi katika maisha yetu ya kila siku. Bwana Swamdaf amesisitiza kwamba, kushiriki kwa wanachuo kutoka nchi mbali mbali za Kiislamu na zisizokuwa za Kiislamu katika mashindano hayo kunaweza kuwa na athari muhimu katika kutatua matatizo ya Waislamu, kuwafahamisha mafundisho muhimu ya Qur’ani na wakati huohuo kuwaunganisha Waislamu wa madhehebu mbalimbali duniani. Amesema, kuhudhuria mashindano hayo wasomaji mashuhuri wa Qur’ani kama vile Sheikh Abul Ainein Sheisha na Ahmad Ahmad Nuaina ni jambo linalotoa motisha na mvuto maalumu kwa washindani wanaoshiriki katika mashindano hayo. Ni vyema kukumbusha hapa kwamba wawakilishi wa usomaji Qur’ani kutoka nchi 40 za dunia wanashiriki katika mashindano hayo ya siku nne ambayo yalianza jana Jumatatu mjini Tehran. 318531