IQNA

16:33 - August 16, 2026
Habari ID: 3482631

Kambi ya Qur’ani yaandaliwa katika kisiwa cha Mahibadhoo, Maldives

IQNA – Kambi inayojumuisha mashindano matatu ya usomaji wa Qur’ani (Tilawa), warsha za ufundishaji, na hafla maalum ya watoto imepangwa kufanyika huko Mahibadhoo, mji wa kisiwani ulioko katikati mwa nchi ya Maldives.

maldivi

Chuo cha Manfaa Academy kimejiandaa kuwa mwenyeji wa kambi hiyo ya Qur’ani.

Makamu wa Rais wa Manfaa Academy na meneja wa kambi hiyo, Mohamed Thaufeeq Ali, amesema kuwa shughuli hizo, zinazofanyika chini ya jina la “Kambi ya Qur’ani ya Manfaa” (Manfaa Quran Camp), ziko wazi kwa wakazi wa Mahibadhoo na visiwa vingine, na zitaendelea kuanzia tarehe 26 hadi 28 mwezi huu. Kwa mujibu wa Thaufeeq, wasomaji mahiri wa Qur’ani (Qari) watahudhuria ili kuongoza warsha, kutoa mihadhara, na kuwa majaji katika mashindano hayo wakati wa kambi hiyo.

“Programu nyingi zinazohusiana na Qur’ani zitaendelea katika kipindi hiki. Ndio maana inaitwa kambi, kwa sababu shughuli mbalimbali zimejumuishwa ndani yake. Wasomaji wengi maarufu wa Qur’ani kutoka Maldives watashiriki. Usomaji wao utasikika, na kutakuwa na warsha zitakazoongozwa na wasomaji hao,” alisema Thaufeeq.

Kambi hiyo itaendeshwa huko Mahibadhoo kwa msaada wa baraza la kisiwa hicho, Kituo cha Elimu cha Atoll (ADh. Atoll Education Centre), na mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali (NGOs).

Shughuli zitakazojumuishwa katika Kambi hiyo ni:

  • Mashindano matatu ya usomaji wa Qur’ani kwa kutazama (Tilawa).
  • Warsha ya kufundisha usomaji mzuri wa Adhana, kwa ajili ya maimamu wa atoll na makhatibu vijana.
  • Warsha maalum kwa waalimu kuhusu mambo ya kuzingatia katika ufundishaji wa Qur’ani.
  • Warsha kwa umma kuhusu usomaji wa Qur’ani kwa mujibu wa sheria za Tajweed.
  • Madarasa kwa ajili ya wanafunzi na makhatibu vijana.
  • Hafla maalum ya watoto.
  • Mihadhara iliyo wazi kwa umma.

Kwa mujibu wa Thaufeeq, wakati ushiriki katika mashindano ya Qur’ani utafanyika kwanza kwa njia ya mtandao kupitia programu maalum (application), mchujo wa washiriki 30 bora utafanyika ana kwa ana huko Mahibadhoo.

Pia alibainisha kuwa zawadi nono zitatolewa kwa washindi katika mashindano yote matatu. Thaufeeq alieleza kuwa hafla ya watoto itajumuisha michezo inayolenga kuwajengea watoto mapenzi na ukaribu na Qur’ani. Hafla hiyo pia itatoa fursa kwa watoto kuuliza maswali na kupata maarifa kutoka kwa wasomaji wa Qur’ani watakaokuwepo.

Manfaa Academy inaendeshwa na Shirika la Manfaa, ambalo lilianzishwa na Ali Rameez.

 3498664

Kishikizo: maldives qurani tukufu
captcha