IQNA

Sauti na lahani nzuri, chanzo cha kuwavutia wasiokuwa Waislamu wazingatie Qur’ani

9:21 - November 13, 2008
Habari ID: 1707726
Sauti na lahani nzuri ya usomaji Qur’ani ni mwanzo wa kuwavutia watu wasiokuwa Waislamu na kuwafanya wakizingatie kitabu huki kitakatifu cha Mwenyezi Mungu.
Kila mara kitabu hiki kinaposomwa, usomaji wake humvutia kila mtu anayekisikiliza, na hii inatokana na ukweli kwamba maneno yaliyomo humo ni ya Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo inafaa kitabu hicho kusomwa kwa njia ya kuvutia na inayofaa ili kuwafanya wasikilizaji wake wavutiwe na hivyo kuweza kuwaathiri zaidi.
Hayo yamesemwa na Abdul Mu’min Ibrahim Suleiman, msomaji wa Qur’ani, raia wa Nigeria ambaye yuko humu nchini kwa ajili ya kushiriki katika duru ya pili ya mashindano ya Qur’ani kwa wanchuo wa Kiislamu. Abdul Mu’min amesema kwamba, Wasilamu wanapasa kuyaweka maneno ya kitabu kitakatifu cha Qur’ani na mafundisho mengine ya Kiislamu katika matendo ya maisha yao ya kila siku. Amesema kinyume na hivyo, Muislamu atakuwa hafai kuitwa Muislamu kwa sababu Uislamu wake utakuwa ni wa jina tu bila ya vitendo. Akitathmini duru hii ya pili ya mashindano ya kimatifa ya Qur’ani Tukufu kwa wanachuo wa Kiislamu, Abdul Mu’min amesema kuwa kiwango cha mashindano hayo ni cha juu sana na kuongeza kuwa kushiriki kwa wasomaji na marefa wa nchini Misri katika mashindano hayo ni dalili ya wazi kwamba mashindano hayo ni ya kuzingatiwa kimataifa. Amewasifu viongozi wa Iran kwa kuandaa mashindano hayo kwa kiwango cha kimataifa na kuongeza kuwa washiriki wa mashindano hayo wamevutiwa sana na ukaribishaji pamoja na mapokezi mazuri waliyopata kutoka kwa wenyeji wao Wairani. Abdul Mu’min Ibrahim ambaye anashiriki katika mashindano ya Tehran kwa mara ya kwanza, amesema mashindano hayo yana umuhimu mkubwa kwa sababu yanawaunganisha Waislamu wa madhehebu zote za Kiislamu na kupunguza chuki na uadui miongoni mwao. Amesema, Waislamu wanapotambua kwamba wana kitabu kimoja tu cha Qur’ani na kwamba Muhammad ndiye Mtume wao wa Mwisho, hapatakuwepo tena na sababu ya wao kugombana bali watazingatia umoja na mshikamano miongoni mwao. Amesema kimsingi hitilafu zinazoonekana miongoni mwa Waislamu zinatokana na kutotambua kwao vyema mafundisho ya kitabu hiki cha mbinguni. Amesema kuwa kwa mtazamo wake, marehemu Ustadh Abdul Basit ndiye msomaji bora zaidi wa Qur’ani lakini akaongeza kuwa, pamoja na kuwa hadi sasa hakuna msomaji ambaye ameweza kumfikia msomaji huyo kwa ujuzi na sauti yake nzuri ya usomaji Qur’ani, lakini bado kuna wasomaji wengi tu mashuhuri na wajuzi wa usomaji Qur’ani akiwemo Shahat Anwar. 319226

captcha