Mwakilishi wa Misri, Nafeh Abdulrahman al Daib amezungumza na ripota wa Shirika la Habari la Kimatiafa la Quran IQNA na kusema kuwa: 'Jitihada za wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuandaa mashindano ya kimataifa ya Quran zimekuwa zikishuhudiwa kwa miaka kadhaa sasa. Suala hili limekuwa na mchango mkubwa katika kuinua motisha ya Makarii na Mahafidhi wa Quran kutoka nchi za kigeni na hivyo kuwapa msukumo zaidi wa kushiriki katika mashindano ya Quran yanayoandaliwa na Iran'.
Amesema, utaratibu wa mashindano hayo ni wa hali ya juu na kuongeza kuwa: 'kuteuliwa majaji wa kimataifa wa Quran kutoka nchi mbali mbali kusimamia mashindano kama vile Abul Einein Sheisha na Ahmad Nuaina ni moja kati ya sababu zilizopelekea mashindano haya kuwa na kiwango cha juu'.
Mwanchuo huyo maarufu wa masomo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Al Azhar mjini Cairo ameashiria kualikwa na kuenziwa makarii mashuhuri duniani katika mashindano ya kimataifa ya wanachuo Waislamu mjini Tehran na kusema kuwa: "Abul Einein Sheisha" wa Misri na Ayatullah Mohammad Taskhiri wa Iran ni kati ya waliojitolea katika masuala ya Qurani mbali na kuwa marejeo ya kiroho miongoni mwa Waislamu. Mwanachuo huyo wa Misri amesema kuwa, 'kufanyika mashindano ya Qurani ya wanahuo ni jambo litakalokuwa na athari muhimu katika kuleta umoja wa Kiislamu mbali na kuwafanya Waislamu wa mataifa mbali mbali kukutana na kujuana. Amesema, mashindano hayo yatazidisha mahaba miongoni mwa Waislamu.
Nafeh Abdulrahman al Daib alizaliwa mwaka 1979 katika mji Kom Hamada mkoani El Bahira nchini Misri. Ni mwanachuo katika Chuo Kikuu cha Al Azhar cha Misri na amewahi kupata nafasi za juu katika mashindano ya kitaifa qiraa ya Qurani Tukufu. 320043