Lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ni kukifahamisha kizazi cha vijana wa nchi hiyo uhakika wa mafundisho ya Kiislamu na kuwalinda Waislamu wa nchi hiyo dhidi ya fikra potofu, mielekeo ya kupindukia mipaka na ugaidi. Mpango wa kuanzishwa kituo hicho ulipitishwa juzi katika mazungumzo ya meya wa mji wa Sofia na mufti mkuu wa Bulgaria. Katika mazungumzo hayo, Abbas Haji, Mufti Mkuu wa Bulgaria amesema kuwa, Waislamu wanapasa kueneza fikra za usamehevu na misimamo ya wastani ili kuwafundisha vijana namna ya kukabiliana na misimamo mikali na ya kupindukia mipaka. Meya wa Sofia pia alisema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho cha kiislamu kitawapa Waislamu fursa ya kuijua zaidi dini yao ili kuwawezesha kuwafundisha watu wengine mafundisho sahihi ya dini hiyo. Shughuli za ujenzi wa kituo hicho muhimu cha Kiislamu zitagharamiwa na Umoja wa Nchi za Kiislamu OIC na shughuli zake za mafunzo kusimamiwa na Wizara ya Elimu na Malezi ya Bulgaria. 322132