IQNA

Umoja na mshikamano wa Waislamu, bishara ya kuenea Uislamu duniani kote

14:35 - November 24, 2008
Habari ID: 1712097
Umoja na mshikamano wa Kiislamu hususan kati ya wanafikra na wanasiasa katika ulimwengu wa Kiislamu utaharakisha mwenendo wa kuenea dini hiyo ya Mwenyezi Mungu duniani kote.
Hayo yamesemwa na Kiongozi wa msafara wa Hija wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Muhammadi Reyshahri katika mazungumzo yake na Sheikh Ibrahim Jaa, kiongozi wa msafara wa Hija wa Senegal ambaye alitembelea ofisi ya Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mjini Madina.
Ayatullah Reyshahri ameashiria hofu ya maadui juu ya kuenea mafundisho ya Uislamu kote duniani na akasema, maadui wa Uislamu wanafanya njama mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzusha hitilafu na kuwatenganisha wafuasi wa dini hiyo ili kuzuia wimbi la kuenea Uislamu duniani kote.
Ayatullah Reyshahri amesema, kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu na miongozo ya hayati Imamu Khomeini na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, moja ya malengo muhimu ya ibada ya Hija ni kuzikurubisha pamoja nchi za Kiislamu. Amesisitiza kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Qurani, manufaa ya ibada ya Hija si ya mtu binafsi pekee bali ibada hiyo ina maslahi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa Waislamu wote. Sheikh Muhammad Reyshahri amesema, uzoefu umeonyesha kwamba, mikutano kama hiyo imepelekea kuimarika zaidi uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi nyingine za Kiislamu.
Mwakilishi wa Faqihi Mtawala na Kiongozi wa msafara wa mahujaji wa Kiirani amesema, ana matumaini kwamba mazungumzo na mikutano ya viongozi wa nchi mbili za Iran na Senegal itakuwa utangulizi wa kustawishwa uhusiano kati ya Tehran na Dakar.
Kwa upande wake Kiongozi wa msafara wa Hija wa Senegal Sheikh Ibrahim Jaa ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwasaidia na kuwaunga mkono Waislamu kote duniani. Sheikh Jaa amesisitiza juu ya kuimarishwa umoja na mshikamano wa Kiislamu katika kipindi cha sasa ambapo maadui wanafanya njama dhidi ya dini hiyo. Amesema kuwa hija ni fusra nzuri ya kubadilishana habari na uzoefu kati ya jumbe za Hija za Iran na Senegal na kujadili masuala ya ulimwengu wa Kiislamu. 324387
captcha