IQNA

Mantiki, jawabu muafaka mbele ya hujuma za vyombo vya habari vya Wamagharibi

10:08 - November 25, 2008
Habari ID: 1712322
Vyombo vya habari vya Magharibi vinatumia mbinu mbali mbali za kisaikolojia kuuhujumu Uislamu halisi wa Mtume Muhammad SAW na kwa hivyo Waislamu kutegemea mantiki ndio njia bora zaidi ya kukabiliana na hujuma hiyo.
Dina Rayan mwandishi wa gazeti la Al Ahram la Misri ambaye alikuwa akishiriki katika Maonyesho ya 15 Kimataifa ya Vyombo vya Habari hapa Tehran ameliambia shirika la IQNA kuwa: 'Nchi za Kiislamu zinapaswa kukabiliana na hujuma ya propaganda za Wamagharibi dhidi ya Uislamu kwa kutegemea mantiki, subira na utulivu'. Amesema Waislamu wanapaswa kujiepusha na vitendo visivyofaa katika kukabiliana na hujuma za Wamagharibi.
Mwanahabari huyo wa Misri ameongeza kuwa, ' Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW alitumia hoja na hekima katika kujadiliana na makafiri na maadui wa Uislamu na kwa hivyo Waislamu wanapaswa kumchukua Mtume kama kigezo katika kukabiliana na Wamagahribi'.
Dina Rayan amesema, jamii ya Kiislamu inahitajia kuanzisha chombo kimoja cha habari cha Kiislamu ambacho kitawajumuisha wasomi Waislamu . Amesema, chombo hicho, kwa ushirikiano wa taasisi kama vile Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, kinaweza kuendesha shughuli nyingi za kuonyesha taswira sahihi ya Uislamu.
Mwandishi habari huyu wa Misri amesisitiza kuwa kuna umuhimu sana wa kuwepo umoja na mshikamano katika Ulimwengu wa Kiislamu ili kuvunja njama za Wamagharibi. Ameashiria sisitizo la Qur'ani Tukufu kuhusu umoja katika Sura ya Al Imaran aya ya 103 isemayo : " Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu". Amesema, Waislamu hawapaswi kuzingatia hitilafu za kimadhehebu, kikabila au rangi bali wanapaswa kwa pamoja kupeperusha bendera ya "La ilaha illa Allah Muhammadun Rasullulah" yaani "Hakuna Apasaye Kuabudiwa ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah".
324971
captcha