Gazeti la Misri la al-Akhbar limesema kikao hicho pia kitachunguza na kujadili mpango wa OIC kuhusu hali ya maisha ya wanawake wa Kiislamu katika jamii za Kiislamu. Sheria zinazowahusu wanawake wa Kiislamu, kuimarishwa nafasi yao katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa, kuwaunga mkono wanawake katika mapambano yao dhidi ya vitendo vya utumiaji nguvu, ubaguzi na kuzingatia masomo yao ni masuala mengine yatakayopewa uzito katika kikao hicho. Ikamludeen Ihsanoghlou, Katibu Mkuu wa OIC amesema kuhusu jambo hilo kwamba, inatarajiwa kwamba kikao cha Cairo kitapitisha utangulizi wa mpango wa umoja huo kuhusiana na kuarifisha na kutambulisha nafasi ya wanawake katika jamii ya Kiislamu. Amesema katika hali ya hivi sasa, wanawake wanaunda nusu ya jamii na kwamba ni kiungo muhimu katika jamii ya Kiislamu. Amesema, wanawake ambao wanalinda na kulea jamii ya baadaye ni nguzo muhimu katika umma wa Kiislamu na kwamba nafasi yao hiyo inapasa kuheshimiwa na kuenziwa. Amesema katika kikao cha tatu cha dharura cha viongozi wa nchi za Kiislamu kilichofanyika mwaka 2005 huko katika mji mtakatifu wa Makka, washiriki walichunguza umuhimu wa nafasi ya mwanamke wa Kiislamu katika jamii, ambapo walipasisha vipengee 10 vya kuimarisha sheria zinazolinda haki za mwanamke wa Kiislamu katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni, kijamii na Kisiasa. Mpango huo unazingatia thamani za usawa na uadilifu katika mafundisho ya Kiislamu na kumuunga mkono mwanamke katika kukabiliana na vitendo vyote vya utumiaji nguvu na ubaguzi dhidi yake. Kikao cha kwanza kama hicho cha Cairo kilifanyika mwezi Novemba 2006 huko Istanbul Uturuki. 324921