IQNA imenukuu habari ya kituo cha intaneti cha Sauti ya Iraq kwamba katika mchezo huo uliopewa jina la “First to Fight” mchezaji anapaswa kuharibu na kuangamiza msikiti, kuuwa watu waliomo na kurarua Qur’ani Tukufu kwa shabaha ya kupata pointi.
Vilevile ili kushinda mchezo huo, mchezaji analazimika kufyatulia risasi nakala za Qur’ani ziliko ndani ya msikiti huo na mchezo huo umebuniwa kwa namna ambayo ili kuweza kupanda na kuingia awamu nyingine, mchezaji analazimika kurarua Qurani na kuharibu misikiti.
Kusambazwa mchezo huo wa komputa katika masoko ya Saudi Arabia na nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi ni hatua nyingine ya kebehi na uvunjaji wa heshima wa makundi yenye kinyongo na Uislamu na Qur’ani Tukufu. Baadhi ya wachambuzi wanakihusisha kitendo hicho na makundi ya Kiwahabi na yanayowakufirisha Waislamu.
Baadhi ya raia wa Saudi Arabia wameelezea wasiwasi wao kuhusu mchezo huo wa komputa unaodhalilisha matukufu ya Kiislamu katika maduka ya nchi hiyo na wameitaka Wizara ya Miongozo ya Kiislamu ya nchi hiyo kufuatilia kadhia hiyo.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa shirika la Sonny la Japan mwezi Oktoba mwaka huu lilisambaza mchezo wa komputa uliokuwa na muziki wa maneno ya Qur’ani ambao shirika hilo lililazimika kuuondoa masokoni baada ya ukosoaji na malalamiko makubwa ya Waislamu. 325125