IQNA

Qur'ani ndio mpango kamili zaidi wa kukabiliana na changamoto

13:59 - November 25, 2008
Habari ID: 1712596
Silaha hatari zaidi ya maadui katika kukabiliana na umma wa Kiislamu ni kuzusha mifarakano miongoni mwa Waislamu. Katika upande mwingine, Qur'ani Tukufu ndio mpango kamili zaidi wa kukabiliana na changamoto mbalimbali na kushikamana na kitabu hicho kitukufu kutapelekea kusambaratika njama zote za maadui za kuzusha fitina za kimadhehebu miongoni mwa Waislamau.
Hayo yamesemwa na Mufti Mkuu wa zamani wa Australia Sheikh Tajudin al-Hilali ambaye pia ni mwanachama wa Baraza Kuu la Mwito wa Kiislamu na vile vile mwanachama wa Jumuiya ya Kikurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu. Katika mahojiano maalumu na IQNA, Sheikh Tajudin al-Hilali amesisitiza juu ya umuhimu wa kushikamana na Qur'ani kama marejeo ya kimsingi ya sheria za Kiislamu.
Mufti huyo wa zamani wa Australia amenukulu Imam Ali AS alipomuuliza Mtume SAW: 'Iwapo fitina zitatokea katika umma ni njia gani ya kujikwamua kutokana na fitina hizo?. Mtume SAW alijibu kwa kusema: "Kitabu cha Mwenyezi Mungu SWT; Ndani yake kuna habari za kabla yenu, mambo ya baada yenu na sheria zinazohukumu baina yunu. Ni kamba madhubuti ya Menyezi Mungu, neno lake la hikima na njia nyoofu. Tutasema kweli iwapo tutatumia Qur'ani, tutatenda uadilifu kama tutahukumu kwa mujibu wake na tutaongoka kama tutashikamana nayo."
Maneno hayo ya Mtume SAW yanabainisha hadhi na utukufu wa kitabu hicho kitukufu na kwamba Qur'ani ni roho na hakuna mwili usiokuwa na roho isipokuwa uliokufa.
Mwanachuoni huyo amesema, ni jambo la kusikitisha kuona kuwa Umma wa Kiislamu umebaki nyuma katika hali ambayo aya ya kwanza ya wahyi iliyomteremkia Mtume katika Qur'ani Tukufu ilikuwa ni "Iqra" yaani soma. Amesema, kuna maamrisho mengi katika Qur'ani ambayo yakizingatiwa umma wa Kiislamu utapata ezi, heshima na karama. Amesema, kama ambavyo Mwenyezi Mungu amefaradhisha Swala na Saumu kwa Waislamu maamrisho yafuatayo matatu pia iwapo hayatatekelezwa umma wa Kiislamu hauwezi kupata ezi na karama.
Awali kabisa ni aya ya 103 ya Sura Al Imran isemayo "Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu".
Pili ni aya ya pili katika Suratul Maida inayosema: "… Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui…"
Na tatu ni aya ya 60 ya Suratul Anfal isemayo: "Basi waandalieni nguvu kadiri muwezavyo…". Lakini la kusikitisha ni kuwa Waislamu leo katika kupambana na maadui wa Mwenyezi Mungu hawashirikiani ipasavyo.
Amekumbusha kuwa nchi za Ulaya ziliamua kubuni Umoja wa Ulaya na sarafu ya pamoja ya Euro ili kukabiliana na sarafu ya Marekani ya dola. Amesema, nchi za Ulaya zimeweza kuungana pamoja licha ya kuwa na dini, rangi, kaumu na tamaduni tafauti.
Sheikh Tajudin al-Hilali ametaka utamaduni wa ezi ukuzwe miongni mwa vijana Waislamu. Amesema kuwa kizingiti hatari zaidi katika kupata ezi na silaha hatari zaidi ya maadui mbele ya umma wa Kiislamu ni silaha ya kuzusha mifarakano. Amesema, 'tunashuhudia Marekani, nchi ambayo Imam Khomeini (SA) aliitaja kuwa ni Shetani Mkubwa, ikipanga njama ya Mashariki ya Kati Mpya kwa lengo la kuupokonya umma wa Kiislamu utambulisho wake.
Sheikh Tajudin al-Hilali amewausia vijana wa Kiislamu kukabiliana na fitina hizo za maadui. Mwanachuoni huyo amewausia Waislamu wote kuwa, siri pekee ya ushindi wa Umma wa Kiislamu ni umoja miongoni mwa Waisalmu. 323148

captcha