IQNA

Taasisi ya Kiislamu ya 'Kutetea Haki za Wanawake' yaanzishwa

10:56 - November 27, 2008
Habari ID: 1713218
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiislamu ambao wameshiriki katika kikao cha pili cha kimataifa huko mjini Cairo Misri, kilichofanyika chini ya anwani ya 'Nafasi ya Wanawake katika Ustawi wa Nchi za Kiislamu', siku ya Jumanne waliamua kuunda taasisi ya kutetea haki za wanawake.
Kwa mujibu wa gazeti la Misri la al-Akhbar pendekezo la kuundwa taasisi hiyo lilitolewa na Ahmad Abu Gheit, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na kukaribishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Umoja wa nchi za Kiislamu OIC. Naila Jabr, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri anayeshughulikia masuala ya mashirika ya kigeni nchini humo amesema kuwa, lengo la kuundwa taasisi hiyo ni kuwashirikisha wanawake katika shughuli mbalimbali za maisha katika jamii, kuwashirikisha katika ustawi wa nchi za Kiislamu na kuwaandalia mazingira yanayofaa ya utulivu wa kiroho na kinafsi pamoja na nafasi za ajira. Amesema, makao makuu ya taasisi hiyo yatakuwa mjini Cairo na kwamba kupitia uwanachama wao katika taasisi hiyo, nchi za Kiislamu zinaweza kutoa michango yao ya kuboreshwa nafasi ya mwanamke katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kijamii, kidini na kiutamaduni. Wawakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa, Unicef, Mfuko wa Ustawi wa Kijamii na vilevile Mfuko wa Ustawi kwa ajili ya Wanawake wa umoja huo Unifem pia walishiriki katika kikao hicho cha siku mbili kilichomalizika siku ya Jumanne mjini Cairo. 326209
captcha