Kwa mara ya kwanza kabisa taasisi inayohusika na masuala ya kidini ya Uturuki imekubali kutarjumiwa Qur’ani katika lugha ya Kikurdi. Akizungumzia suala hilo, Muhammad Gormiz, Mkuu wa Taasisi ya Masuala ya Kidini ya Uturuki amesema kuwa, kufuatia hatua ya televisheni ya serikali ya nchi hiyo TRT ya kutangaza matangazo kwa lugha ya Kikurdi, taasisi hiyo pia imeamua kuruhusu kutarjumiwa kwa Qur’ani kwa lugha hiyo.
Ameongeza kuwa, uhaba wa wataalamu na watarjumi mahiri wa lugha hiyo na Kiarabu nchini Uturuki ndicho kikwazo kikuu kinachozuia kutekelezwa jukumu hilo muhimu.
Katika upande wa pili, mkuu wa idara inayosimamia magazeti ya Uturuki amesisitiza umuhimu wa kutarjumiwa Qur’ani katika lugha tofauti na kuongeza kuwa, lugha ya Kikurdi ni moja ya lugha zilizoenea sana nchini humo na kwa hivyo kutarjumiwa Qur’ani kwa lugha hiyo inayozungumzwa na watu wengi nchini Uturuki, kuna umuhimu mkubwa.
Inasemekana kwamba taasisi hiyo ya masuala ya kidini imetuma wahubiri wengi wa Kiislamu katika maeneo ya Wakurdi ya kusini mashariki mwa nchi hiyo ili kuwafahamisha Wakurdi utamaduni wa Kiislamu.
Lugha ya Kukurdi imepigwa marufuku kufundishwa katika shule za msingi na vyuo vikuu vya nchi hiyo. 328356