Swaleh At'hari Fard, mshindi wa kwanza wa mashindano ya kimataifa ya usomaji Qur'ani ya mwaka huu, amekosoa vikali muamala wa askari wa kidini na usalama wa Msikiti wa Haram kwa wasomaji Qur'ani waliohudhuria shughuli ya usomaji Qur'ani katika Taasisai ya Kiongozi Muadhamu inayoshughulikia masuala ya mahujaji wa Iran nchini Saudi Arabia.
At'hari Fard amemwambia mwandishi wa IQNA mjini Makka kwamba askari hao wanatumia njia mbalimbali za kuwaudhi wasomaji Qur'ani ikiwa ni pamoja na kuwapiga picha kwa nguvu, kuwatia hofu kwa kupiga mayowe, kuwasukuma ovyo wanaposoma Qur'ani, kuvuta mazulia wakiwa wameketi au kusimama, kutoiheshimu Qur'ani kwa kutumia visingizio kama vile vya kutaka kuosha sehemu Qur'ani inakosemewa, lengo lao kuu likiwa ni kuvuruga shughuli zao za usomaji wa kitabu hicho kitakatifu. Msomaji huyo amesema kuwa, wanaolengwa hasa katika vitendo hivyo vya dharau ni Wairani kwa sababu mahujaji wengine wanaokuwa na shughuli kama hizo huwa hawakabiliwi na dharau kama hiyo kutoka kwa Wasaudi, bali hata husaidiwa kuendesha shughuli zao bila matatizo yoyote. Inasemekana kuwa, mahujaji wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia hukusanyika katika sehemu wanayosomea Qur'ani mahujai wa Iran na kuvutiwa sana na usomaji wao wa kitabu hicho. Jambo hilo limepelekea kuvunjwa njama zote zinazoenezwa na Mawahabi wa Saudia dhidi ya Wairani na mfumo wa Kiislamu wa serikali ya Iran. Kutokana na propaganda sumu zinazoenezwa na Wasaudi dhidi ya Iran, Wasunni wengi hudhani kwamba Qur'ani haipewi umuhimu wowote nchini Iran na hata kwamba kuna Qur'ani tofauti kabisa inayochapishwa nchini Iran. Tokea tarehe Mosi Dhul Hija na kwa muda wa usiku tano, wasomaji Qur'ani wa Iran wamekuwa wakisoma Qur'ani Tukufu katika orofa ya pili ya Masjidul Haram. 328822