IQNA

Filamu ya Fitna kuonyeshwa Marekani na Uingereza

12:55 - December 10, 2008
Habari ID: 1717690
Mwenyekiti wa chama cha Uhuru cha Uholanzi na mbunge mwenye misimamo ya kufurutu mipaka wa nchi hiyo Geert Wilders amesema kuwa filamu ya Fitna inayokivunjia heshima kitabu cha Qur'ani na matukufu ya Kiislamu itaonyeshwa katika nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa na katika utawala ghasibu wa Israel.
Wilders amesema, atafanya safari katika nchi kadhaa duniani kwa ajili ya kuasisi mkataba wa kimataifa wa kupiga vita mwamko wa Kiislamu.
Geert Wilders alionyesha filamu ya Fitna inayokidhalilisha kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika mtandao wa intaneti mwaka uliopita. Filamu hiyo inaitaja Qur'ani kuwa ni kitabu cha kifashisti na anaonekana humo akichoma moto baadhi ya aya za Qur'ani.
Filamu hiyo ya dakika 16 inaanza kwa picha za vijikatuni vya mchoraji wa Denmark vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) na inajumuisha taswira mbaya za mauaji ya kikatili zilizowekwa kandokando ya aya za Qur'ani Tukufu. Filamu hiyo pia inautaja Uislamu kuwa ni hatari kubwa kwa uliberali, uhuru na thamani za Kimagharibi.
Geert Wilders ni mwanasiasa wa mrengo wa kulia mwenye misimamo ya kufurutu mipaka anayewapiga vita wahajiri wa Kiislamu. Mwanasiasa huyo amekuwa akiendesha harakati zilizodhidi ya Uislamu na Qur'ani Tukufu. 332061
captcha