Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA mjini Amman, wasomi na wananchi wa Jordan wameitaka serikali ya Misri kuchukua hatua za haraka kuhakikisha njia ya mpakani ya Rafah inafunguliwa ili kuwaondolea masaibu Wapalestina walio katika mzingiro wa Wazayuni huko Gaza.
Katika mahojiano na kanali ya Al Alam, Azzam al Hindi, mwakilishi wa Harakati ya Amal Islami katika bunge la Jordan amesema: "Mzingiro wa Gaza unaashiria jinai ambazo hazijawahi kushudiwa katika historia".
Ameongeza kuwa, 'Watu milioni moja na nusu wanaishi katika mzingiro huo wa kinyama na mbali na kuharibiwa nyumba zao, vile vile wamenyimwa chakula". Mbunge huyu wa Jordan amesisitiza kuwa mzingiro wa Gaza unaonyesha namna Wamagharibi wanavyowahadaa walimwengu wanapodai eti wanatetea haki za binadamu.
Naye Ibrahim Dabur, mmoja wa makasisi wa Jordan amesema: Hakuna dini yoyote inayoidhinisha mzingiro kama unaoshuhudiwa huko Gaza. Naye Profesa Ahmad Nufel mhadhiri wa sayansi ya siasa katika cChuo Kikuu cha Yarmuk cha Jordan amesema: "Wapalestina katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na mkasa wa kihakika wa ukosefu wa uthabiti, usalama na chakula cha kila siku. Aidha ametoa wito kwa serikali ya Misri kuzingatia ubinadamu na kuwasaidia Wapalestina kisiasa.
Mwananchi mmoja wa Jordan amesema nchi za Kiarabu na Kiislamu zinapaswa kutuma misaada ya dharura huko Gaza haraka iwezekanavyo. Amesema, ni jambo lisilokubalika kwa Waislamu zaidi ya bilioni moja na nusu duniani kushindwa kuwasaidia Wapalestina milioni moja na nusu wanaokandamizwa na Wazyauni huko Gaza. 335869