Hassan Qashqavi amelaani vikali mashambulizi ya pande zote yaliyofanywa na ndege za kivita za Israel dhidi ya Gaza, na kuitaka jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu pamoja na nchi zote za Kiislamu, kuchukua hatua za haraka ili kuzuia jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha ametoa pole kwa taifa la Palestina kwa tukio hilo la kusikitisha na kutangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwa pamoja na taifa madhlumu la Palestina katika kukabiliana na siasa za kujipanua za utawala wa kigaidi wa Israel.
Kwa upande mwingine Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesisitiza kuwa utawala ghasibu wa Israel utalipa gharama kubwa kwa kuwaua kwa umati wakazi wasiokuwa na hatia na wanaozingirwa wa Ukanda wa Gaza.
Rais Ahmadinejad alaani mauaji ya Gaza
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amelaani vikali mauaji ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza akasisitiza kuwa jinai hiyo itazidisha uzito wa faili chafu la Wazayuni na kuifanya mbaya zaidi hatima yao.
Rais Ahmadinejad ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na kiongozi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina Dakta Ramadhani Shalah na akatoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi waliouawa kinyama katika mashambulizi ya jana ya Israel. Amesema kuwa taifa la Iran limesikitishwa mno na tukio hilo na limo katika maombolezo na kwamba litaendelea kuwa pamoja na wananchi wa Palestina.
Rais Ahmadinejad amesisitiza juu ya kuendelezwa mapambano ya ukombozi ya wananchi wanaokandamizwa wa Palestina na akasema: Mapambano ndiyo yanayoweza kuvunja mgongo wa utawala ghasibu wa Israel na kuwakatisha tamaa Wazayuni.
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel ambalo limewaua kinyama zaidi ya Wapalestina 230 katika kipindi cha masaa 12 kuanzia jana, limeshambulia na kubomoa pia msikiti wa eneo la al Rimal. Shambulizi hilo limeua watu kadhaa na kujeruhi wengine wengi ndani ya msikiti huo.339109