Baada ya kupita siku tano za mashambulio ya kinyama yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza kwa ushirikiano wa watawala wa Misri, Rais Husni Mubarak wa nchi hiyo amejitokeza na kutangaza kile amedai kwamba ni juhudi za nchi hiyo za kusaidia kumaliza mgogoro wa ukanda huo.
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa ya Misri kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya wa Hijiria na vilevile wa Milaadia, Rais Mubarak amejifanya kuwasihi watawala wa Israel wasimamishe mashambulio yao ya kinyama dhidi ya wakazi wasio na ulinzi wa Gaza. Rais huyo amelaani mashambulio hayo ya Gaza na kusema kuwa Israel inapasa kusimamisha mara moja mashambulio hayo katika Ukanda huo. Rais Mubarak amedai kutetea wakazi wa Ukanda wa Gaza katika hali ambayo nchi yake inashirikiana kikamilifu na Wazayuni katika kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina wa ukanda huo na kutoruhusu kabisa misaada ya kibinadamu inayotolewa na nchi za Kiislamu kuwafikia wakazi wa ukanda huo wanaoendelea kuteseka chini ya mashambulio ya kinyama na mzingiro unaotekelezwa dhidi yao na Wazayuni. Jambo hilo limewakasirisha sana Wamisri na kuwafanya wafanye maandamano makubwa ya kupinga siasa za serikali ya Misri ya kushirikiana na Wazayuni katika kuwatesa na kuwaua kinyama ndugu zao wa Palestina. Maandamano hayo yamefanyika licha ya kuwepo marufuku ya serikali ya kutoruhusu kabisa maandamano kufanyika nchini humo dhidi ya mashambulio ya Israel huko Gaza. 341589