IQNA

Makanisa yanajaribu kukomesha mashambulio ya Gaza

9:52 - January 05, 2009
Habari ID: 1727596
Ataullah Hanna, Mkuu wa Makanisa ya Kiorthodox ya Quds Tukufu ametoa taarifa akiyataka makanisa yote ulimwenguni kufanya juhudi za kukomesha mashambulio ya kinyama yanayotekelezwa na Wazayuni dhidi ya wananchi wasio na hatia wala ulinzi huko katika Ukanda wa Gaza.
Hanna Amesema katika taarifa hiyo kwamba, maaskofu na viongozi wote wa Kikristo duniani wanapasa kufanya juhudi za kusimamisha mashambulio ya kinyama na mzingiro wa kidhulma unaotekelezwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina milioni moja na nusu katika Ukanda wa Gaza. Amesema, jinai zinazotekelezwa na Israel katika ukanda huo zimebadilika na kuwa mkasa mkubwa wa kibinadamu, na kwamba mashambulio ya kinyama yanayofanywa na utawala huo ghasibu yanawalenga Waislamu na Wakristo wakazi wa ukanda huo, kwa kadiri kwamba makanisa na misikiti haijasalimika na hujuma hiyo ya Wazayuni.
Hanna ameeleza masikitiko yake makubwa kutokana na kimya cha jumuiya na viongozi mbalimbali wa ulimwengu kuhusiana na jinai zinazotekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza. Amesema kwamba makanisa yanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuwafahamisha watu jinai zinazotekelezwa katika ukanda huo na kuwataka wawasaidie watu wanaoteseka kutokana na jinai hizo. Amesifu msimamo wa wakazi wa Gaza ambao hawajauhama ukanda huo kwa kuhofia mashambulio ya Wazayuni na kusema kuwa hiyo ni ishara ya wazi ya ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Wakristo na Waislamu katika kukabiliana na mauaji ya umati na njama zinazotekelezwa na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Ukanda huo. 343559
captcha