Sheikh Yusuf Kardhawi amewatumia ujumbe Mayahudi wenye misimamo mikali wa utawala wa Kizayuni wa Israel na akasema: Wakati umefika wa kutekelezwa suna ya Mwenyezi Mungu kuhusu madhalimu na kwamba ahadi ya kweli ya kuangamizwa madhalimu wa Kiyahudi inakaribia.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu amezilaumu nchi za Magharibi hususan Marekani kwa kupuuza jinai zinazofanywa na Israel na aksema: Washington haistahiki kuongoza dunia. Amewakosoa vikali pia viongozi wa nchi za Kiarabu kufuatia mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Sheikh Qardhawi amesema, viongozi wa nchi za Kiislamu wamepuuza hali ya wananchi wa Gaza na amewausia kumcha na kumuogopa Mwenyezi Mungu. Sheikh Qardhawi amesema, wananchi wamekwishatoa kauli yao na sasa ni zamu ya viongozi kuwasikiliza.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu amesema kuwa, viongozi wa nchi za Kiarabu wako kama wamepofuka na hawaoni mauaji ya Holocaust yanayofanywa na Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Wanashuhudia kwa macho maafa hayo bila ya kuchukua hatua yoyote. Amesisitiza Sheikh Qardhawi.
Amesema kuwa iwapo hali ya Gaza itaendelea kama ilivyo hivi sasa viongozi wa nchi za Kiarabu hawataendelea kuongoza nchi zao, kwani watapoteza uhalalali wa kubakia madarakani waliopewa na wananchi.
Sheikh Qardhawi amewaambia viongozi wa nchi za Kiarabu kwamba, ni aibu kwao kuona ndugu zao wakiuawa mbele ya macho yao huku wakiwa wamenyamaza kimya. 345365