Kwa mujibu wa ukurasa wa intaneti wa Saut al Iraq, ofisi ya Ayatullah Fayaz katika mji mtakatifu wa Najaf imelaani vikali mauaji ya watu wasio na hatia huko Gaza na kusema, uungaji mkono wa Congress ya Marekani kwa jinai za Wazayuni ni jambo la kuaibisha sana.
Kiongozi huyo wa kidini nchini Iraq amesema kuwa: “Marekani na taasisi za kimataifa zinanyamazia kimya jinai mbalimbali za Wazayuni dhidi ya raia huko Gaza lakini pale Mpalestina mwanamapambano anapokabiliana na Israel na kujihami anatajwa kuwa gaidi”.
“Kukabiliana na dhulma na ukandamizaji wa Wazayuni na juhudi za kukomesha jinai hizo za kukaririwa za Israel ni jukumu la kibinadamu na kimaadili la nchi zote duniani na hasa nchi za Kiarabu na Kiislamu”, amesema Ayatullah Fayaz .
Marjaa huyo wa kidini wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq amemaliza kwa kutoa wito kwa jumuiya za kimataifa na kieneo kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC kuchukua hatua muafaka za kusimamisha mara moja jinai za Israel huko Gaza na kuhakikisha kuwa Wapalestina wanarejeshewa haki zao zote. 347660