IQNA

Kitabu cha 'Mwanamke Katika Uislamu' chachapishwa

9:57 - January 15, 2009
Habari ID: 1731232
Kitabu chenye anwani ya "Mwanamke Katika Uislamu na Nafasi yake katika Jamii" kilichoandikwa na Dr Abdul Rahman Ibn Abdul Aziz Al Tuwaijiri Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO kimechapishwa na kufasiriwa kwa lugha za Kiingereza na Kifaransa.
Kwa mujibu wa taarifa ya ISESCO, katika utangulizi wa kitabu hicho, Dr.Al Tuwaijiri amesema, kitabu hicho kilichapishwa mara ya kwana mwaka 1992 kwa lugha ya Kiarabu lakini baada ya kupita miaka 13 kumejitokeza umuhimu wa kukifanyia marekebisho na kukichapisha upya kwa kuzingatia matukio mbalimbali duniani na vile vile kutokana na mjadala unaoendelea kuhusu mtazamo wa Uislamu kwa mwanamke katika jamii.
"Mjadala kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii ya leo ni kati ya maudhui muhimu zinazojadiliwa kwa wingi. Kwa kuzingatia namna dini tukufu ya Kiislamu ilivyompa thamani mwanamke, kuna udharura kwa mitazamo ya dini hiyo ya mbinguni kuhusu kadhia hii kubainishwa kwa walimwengu", amesema -Dr Al Tuwaijiri.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa ISESCO ameendelea kuashiria nafasi ya kipekee ya mwanamke katika jamii na kusema kuwa, nafasi ya wanawake katika jamii inazidi kuongezeka siku hadi siku. Suala hili linafungua ukurasa mpya kwa watafiti wa masuala ya jamii. "Mjadala kuhusu mwanamke Muislamu na nafasi yake si mada ya kijamii tu bali pia ni ya kisiasa kwani kuna wengi ambao kwa kusoa mtazamo wa Uislamu kuhusu mwanamke wanakusudia kutoa pigo kwa dini hii tukufu". Amesema, ni kwa kuzingatia mitazamo hiyo potofu, ndipo uamuzi ukachukuliwa kuchapisha kitabu hicho ili kufafanua mitazamo halisi ya Uislamu kuhusu mwanamke. "Katika kitabu hiki tunaeleza bayana kuwa haki za mwanamke katika Uislamu zinazingatiwa kikamilifu na kwamba mwanamke Muislamu leo anahusika moja kwa moja katika maamuzi ya kisiasa na kijamii katika nchi yake", amesema -Dr Abdul Al Tuwaijiri. 348268
captcha