IQNA

Shimon Peres apokonywe tuzo ya Nobel

12:13 - January 18, 2009
Habari ID: 1732409
Rais Evo Morales wa Bolivia ameitaka Taasisi ya Nobel impokonye Shimon Peres, Rais wa utawala haramu wa Israel tuzo iliyompa mwaka 1994 kutokana na jinai za utawala huo zinazotekelezwa huko Gaza dhidi ya watu wasio na hatia.
Morales amesema kuwa, tuzo hiyo hutunukiwa watu ambao wametoa mchango katika kuimarisha amani na kwamba Peres hajafanya lolote katika uwanja huo bali ni mtenda jinai na mchochezi wa vita ambaye mikono yake imejaa damu ya watoto na wanawake wasio na hatia. Ameongeza kuwa Peres ni mtenda jinai za kivita ambaye licha ya kuonyeshwa picha hai na za moja kwa moja kupitia televisheni za kimataifa lakini anadai kwamba hakuna watoto wala wanawake wanaouawa katika hujuma ya utawala haramu wa Israel huko Gaza na kwamba wanaouawa katika hujuma hiyo ya kinyama ni wale anaowatuhumu kuwa ni magaidi wa Hamas wanaopasa kupewa funzo!
Evo Morales amesema kwamba nchi yake imeazimia kuzishawishi nchi za Latin Amerika kuwafikisha viongozi wa utawala haramu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kutokana na jinai za kivita dhidi ya watu wasio na hatia. Amesema tayari mazingira ya kuratibiwa rasimu ya mashtaka ya nchi hizo inatayarishwa na kwamba wiki ijayo nchi hizo zitawasilisha mashtaka hayo katika mahakama hiyo ya mjini Hague.
Morales amesema kwamba kwa kuwaua kwa umati watu wasio na hatia na kwa kutumia silaha zilizopigwa marufuku kimataifa utawala haramu wa Israel umekiuka sheria zote za kimataifa kuhusiana na udharura wa kulindwa haki za raia.
Wiki iliyopita Bolivia na Venezuela zilikata uhusiano wao na utawala haramu wa Israel kutokana na hujuma ya kinyama inayoendeshwa na utawala huo dhidi ya watu wasio na ulinzi huko Gaza. 349658
captcha