IQNA

Takwa la wanafikra wa Kiislamu kwa Barack Obama:

Mabadiliko katika sera za White House kuhusu ulimwengu wa Kiislamu

8:30 - January 24, 2009
Habari ID: 1734729
Katika hali ambayo Rais Barack Hussein Obama wa Marekani ndio kwanza amechukua madaraka ya nchi huko Marekani, kundi la wanafikra wa Kiislamu limemwandikia barua likimtaka abadili sera za ikulu ya nchi hiyo White House kuhusu ulimwengu wa Kiislamu.
Gazeti la al Sharq la Qatar limeandika kuwa, barua hiyo imeandikwa na wanafikra 38 wa Kiislamu wakiwemo wanaharakati wa kisiasa na kisheria na wawakilishi wa taasisi na jumuiya mbalimbali za Kiislamu kama Sheikh Yusuf Qardhawi, Mwenyekiti wa Muungano wa Kimataifa wa Maulamaa wa Kiislamu.
Sehemu moja ya barua hiyo imesema: Umma wa Kiislamu ambao unamiliki suhula nyingi za kimaada na kimaanawi na uwezo mkubwa wa dhahiri na usiokuwa dhahiri, utakuwa na nafasi kubwa katika ujenzi wa mustakbali wa dunia hii.
Wanafikra hao wa Kiislamu wamempongeza Barack Obama kwa kuchukua madaraka nchini Marekani na kusisitiza kuwa wanatumia fursa hiyo kuzungumza na Obama kuhusu masuala muhimu yanayozihusu pande mbili kama vile maadili, thamani na haki za binadamu.
Wanafikra hao wa Kiislamu pia wameutaja ushindi wa Obama kuwa ni mafanikio ya kihistoria kwake yeye na wananchi wa Marekani. Wameashiria aya ya pili ya suratul Maidah inayosema: Na saidianeni katika wema na kumcha Mwenyezi Mungu na wala msisaidiane katika maovu na uadui.." na wakaliambia taifa la Marekani kwamba linapaswa kujenga uhusiano na mataifa yote ya dunia kwa ajili ya kufikia maslahi ya pamoja kama amani na ustawi kote duniani na kufanya juhudi za kuondoa hatari na matatizo yanayoukabili ulimwengu.
Sehemu nyingine ya barua ya wanafikra wa Kiislamu kwa Barack Obama imesema: "Sisi Waislamu tunaoshikamana na mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu hatuogopi nguvu yoyote isiyokuwa Mwenyezi Mungu na tunaheshimu haki za dini, tamaduni na makundi yote.
Barua ya wanafikra wa Kiislamu kwa Rais mpya wa Marekani imemalizia kwa kuashiria suala muhimu la ugaidi na njia za kupambana nao na kusisitiza kwamba: Katika dini tukufu ya Uislamu kuua watu wasiokuwa na hatia kunatambuliwa kuwa ni ufisadi na kutenda maovu katika ardhi na moja ya jinai kubwa. Dini hiyo pia inaruhusu vita katika hali ya dharura na kwa ajili ya kulinda haki, kuzuia dhulma sambana na kuchunga thamani za kimaadili na kisheria. 352762
captcha