IQNA

Mashindano ya Qur'ani na hadithi ya wanachuo yaanza Sharjah

13:34 - January 26, 2009
Habari ID: 1735984
Mashindano ya 13 ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu na Hadithi kwa wanachuo kote katika Umoja wa Falme za Kiarabu yameanza nchini humo kwa udhamini wa Taasisi ya Qur'ani Tukufu na Sunna, ya Ufalme wa Sharja katika falme hizo.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Khalij, masindano hayo yatakayoendelea kwa muda wa siku nne yatafanyika chini ya usimamizi wa Sultan bin Muhammad al-Qassimi, mtawala wa ufalme huo. Waandaaji wa mashindano hayo wamesema kuwa yatafanyika katika makundi mawili ya wanaume na wanawake.
Kamati inayosimamia mashindano hayo imetangaza kwamba mashindano ya kuhifadhi Qur'ani yatagawanyika katika sehemu kadhaa za kuhifadhi Qur'ani nzima, kuhifadhi juzuu 20, juzuu 15, juzuu 10 na juzuu 5 na hatimaye kuhifadhi hadithi za Mtume Mtukufu (saw).
Kamati hiyo imesema kuwa lengo hasa la mashindano hayo ni kuimarisha moyo wa mashindano ya kuhifadhi Qur'ani na hadithi kati ya wanachuo pamoja na kuimarisha utamaduni wa Qur'ani na Uislamu katika jamii ya Imarati.
Sherehe za kuwashukuru na kuwatuza washindi wa mashindano hayo zitafanyika miezi minne ijayo. 353722
captcha